Mashtaka dhidi ya kijana wa saa yaondolewa

Haki miliki ya picha Anil Dash
Image caption Ahmed Mohamed

Polisi wa Texas wamemuondolea mashtaka mvulana mwislamu mwenye umri wa miaka 14 aliyekamatwa kwa kutengeza saa.

Maafisa katika shule ya upili ya Mac Arthur mjini Irving waliwaita maafisa wa polisi baada ya kudhania kwamba saa hio ilikuwa bomu.

Kukamatwa kwa Ahmed Mohammed kumekosolewa na wengi huku kijana huyo akipata mwaliko katika ikulu ya White House nchini Marekani.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ahmed na wazazi wake

Ahmed aliwaambia waandishi wa habari kwamba inasikitisha kwamba mwalimu wake alidhania saa hiyo ilikuwa tishio.''Nilitengeza saa ili kumfurahisha mwalimu wangu lakini nilipomuonyesha alidhani ilikuwa tisho kwa maisha yake. Ninasikitishwa kwamba alinidhania vibaya''.

Katika mkutano huohuo na vyombo vya habari,Ahmed amesema kuwa anataka kuihama shule hiyo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ahmed akiwa na saa yake

Babaake kijana huyo Mohammed Elhassan Mohamed ambaye anatoka nchini Sudan,alimsifu mwanawe akisema anatengeza kila kitu ndani ya nyumba yao ikiwemo simu ya babaake na tarakilishi.

''Ni kijana mwerevu sana na kwamba alisema anataka ulimwengu umjue''.Mafisa wa polisi hatahivyo wamekana madai ya familia ya Ahmed kwamba alikamatwa kutokana na jina lake.

''Tumekuwa na uhusiano mzuri na jamii ya waislamu'', alisema mkuu wa polisi wa eneo la Irving Larry Boyd siku ya jumatano.''Visa kama hivi hutoa changamoto.Tunataka kukichukulia kisa hiki kama funzo zuri''.