Croatia yafunga vituo vya kuvukia mpaka

Wahamiaji Croatia Haki miliki ya picha Getty
Image caption Waziri mkuu wa Croatia amesema taifa hilo halina uwezo wa kupokea wahamiaji zaidi

Croatia imefunga vituo saba kati ya vinane vinavyotumiwa kuingia taifa hilo kutoka Serbia baada ya wahamiaji wanaotaka kuingia taifa hilo kuongezeka sana.

Maafisa mjini Zagreb walisema hakuwa na budi ila kufunga vituo hivyo baada ya watu 10,000 kuingia taifa hilo siku moja baada ya Hungary kuweka uzio kwenye mpaka wake na Serbia.

Hayo hakijiri, Slovenia ilisema imezuia kundi la wahamiaji waliokuwa kwenye treni na kwamba itawarejesha Croatia.

Maelfu ya watu ambao wamekuwa wakielekea kaskazini kutoka bahari ya Mediterranean wamesababisha mzozo mkubwa wa kisiasa katika Muungano wa Ulaya.

Maafisa wa serikali nchini Croatia walisema barabara zinazoelekea vituo hivyo vya kuvukia mpaka pia zimefungwa.

Kivuko cha mpakani katika barabara kuu inayounganisha Belgrade na Zagreb - kilichoko Bajakovo – ndicho pekee kilichobaki wazi.

Alhamisi, waziri wa mambo ya ndani wa Croatia Ranko Ostojic alisema taifa hilo limejaa.

Alisema ujumbe wake kwa wahamiaji ni: “Msije hapa tena. Kaeni katika vituo vya wakimbizi Serbia, Macedonia na Ugiriki. Hii siyo barabara ya kuelekea Ulaya. Mabasi hayawezi kuwafikisha huko. Huo ni uongo.”

Waziri mkuu wa Croatia Zoran Milanovic alisema taifa lake lina “uwezo mdogo”.

Vurugu zilizuka katika maeneo mawili katika mpaka wa Croatia na Serbia Alhamisi baada ya watu kusubiri kwa saa nyingi kuapata njia ya kuwasafirisha kaskazini.

Watu walizidi nguvu na kuvuka vizuizi vya maafsa wa polisi kwa muda mfupi katika vituo vya kuvukia mpaka vya Tovarnik na Batina, ambavyo ni miongoni mwa vilivyofungwa baadaye.