Faini barabarani kulipwa kidijitali TZ

Polisi Tanzania
Image caption Dereva ataweza kulipia faini yake papo hapo kwa kutumia simu au kadi ya benki

Polisi nchini Tanzania wamezindua rasmi mfumo wa ulipaji faini za hapo kwa hapo kwa kutumia njia ya kielektroniki kwa dereva yeyote atakayekamatwa na kosa la barabarani.

Kamanda Mohamed Mpinga ambaye ni mkuu wa kitengo cha usalama barabarani nchini humo ameiambia BBC kuwa hatua hiyo inalenga kwenda na teknolojia.

Aidha, imechukuliwa kutokana na raia ambao wamekuwa wakilalamika kwamba hawapewi stakabadhi wanapolipa faini na hivyo kutoa fursa kwa ulaji rushwa.

Mfumo huo mpya umeanza kwa majaribio katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, ambapo takriban mashine 350 vimeanza kutumika kuwalipisha faini madereva wanaopatikana na hatia.

Bw Mpinga amesema hatua hiyo inakusudiwa kuleta usasa, ueledi pamoja na ushirikiano wa jamii.

"Tumekuwa tukipata malalamiko mengi sana ya wananchi kuhusiana na ulipaji wa faini. Mtu kwa mfano anakuwa hana hela, lakini vilevile wamelalamika sana kutopata risiti wanapokuwa barabarani," amesema.

"Kwa upande wa pili, tunaamini mfumo huu utasaidia kuboresha mapato zaidi ya serikali kwa sababu fedha zinakwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya jeshi la polisi.”

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wanaonekana kuipokea hatua hiyo kwa hisia tofauti huku baadhi wakisema hauwezi kupunguzi vitendo vya rushwa.

Hassan Musa ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam na dereva wa teksi anakubali kwamba mfumo huo unaweza kufaa katika kuziba mianya ya rushwa.

Haki miliki ya picha
Image caption Baadhi ya madereva wanaamini mpango huo utapunguza ulaji hongo

Naye Elias John Tupa ambae pia ni dereva wa teksi anaonekana kuwa na maoni tofauti.

"Mimi nimeupokea vizuri, lakini maoni yangu, wangekuwa wameweka kiwango cha makosa, kwamba dereva alipie kosa moja. Lakini nikiandikiwa makosa matatu, hata kama malipo ni kwa njia ya mtandao, bado nitalazimika kumshawishi afisa wa trafiki achukue elfu kumi kama rushwa ili aniachilie."

Tofauti na utaratibu uliopo hivi sasa wa mtuhumiwa kutakiwa kulipia faini hapo kwa hapo, utaratibu mpya utampa fursa dereva kulipia faini yake kwa njia ya simu au kadi ya benki katika kipindi cha siku saba.

Aidha Bw Mpinga amemwambia mwandishi wa BBC Aboubakar Famau kwamba mfumo huu utakwenda sambamba na kanuni ya uwekaji wa nukta katika leseni za udereva kulingana na uzito wa kosa lililotendwa na dereva.