Polisi wazuilia meli bandarini Mombasa

Bandari ya Mombasa
Image caption Bandari ya Mombasa imekuwa ikitumiwa sana na walanguzi kusafirisha mihadarati kutoka Afghanistan

Polisi nchini Kenya wanazuilia meli inayoshukiwa kubeba shehena ya dawa za kulevya katika bandari ya Mombasa.

Kikosi cha maafisa, kiliojumuisha maafisa kutoka kikosi cha kupambana na dawa za kulevya na maafisa wa uchunguzi wa jinai, kilifika katika bandari hiyo ghafla usiku wa manane.

Maafisa hao waliagiza kila mtu kuondoka na kufunga milango yote ya kuingia na kutoka kwenye bandari hiyo.

Operesheni hiyo iliwashangaza hata wasimamizi wa bandari hiyo walioonekana kutokuwa na habari.

Mkuu wa polisi wa Mombasa Francis Wanjohi amethibitisha kwamba wanasaka dawa za kulevya kwenye meli hiyo.

Image caption Polisi wamefunga milango ya kuingia na kutoka bandari ya Mombasa

Bandari ya Mombasa imekuwa kituo muhimu cha kusafirishia dawa za kulevya kutoka Afghanistan kuelekea Ulaya.

Pesa kutoka kwa biashara hiyo zimekuwa zikidaiwa kutumiwa kufadhili makundi ya kigaidi.

Meli za kushika doria baharini chini ya kikosi cha pamoja cha kimataifa zimekuwa mara kwa mara zikinasa meli zilizobeba mihadarati katika Bahari ya Hindi karibu na Afrika Mashariki.

Ingawa visa vingi vya ulanguzi huhusisha boti ndogo, wakati mwingine walanguzi huficha dawa hizo katika meli kubwa.