Wanajeshi Burkina Faso walenga mji mkuu

Gilbert Diendere
Image caption Kiongozi wa mapinduzi ya serikali Jenerali Diendere anataka kuongoza hadi uchaguzi ufanyike

Wakuu wa jeshi la Burkina Faso wamewataka viongozi waliopindua serikali wiki iliyopita kuweka silaha chini, na kutangaza kwamba wanaelekea mji mkuu wa Ouagadougou.

"Wanajeshi wote wa jeshi la taifa wanaelekea Ouagadougou lengo lao pekee likiwa kuwapokonya silaha walinzi wa rais bila umwagikaji wowote wa damu,” wamesema kupitia taarifa.

Mapinduzi ya serikali yaliyomuondoa uongozini rais wa mpito Michel Kafando yaliongozwa na kikosi cha walinzi wa rais.

Hali ya wasiwasi bado imetanda katika mji huo mkuu.

Viongozi wa mapinduzi hayo ni washirika wa karibu wa Rais Blaise Compaore aliyeondolewa mamlakani kufuatia maandamano ya raia mwaka jana.

Bw Compaore kwa sasa anaishi uhamishoni Ivory Coast.

Walinzi hao wa rais walitekeleza mapinduzi hayo baada ya kuvamia mkutano wa baraza la mawaziri Alhamisi iliyopita uliokuwa ukiongozwa na Rais Kafando na Waziri Mkuu Isaac Zida Alhamisi.

Rais Kafando aliachiliwa huru baadaye lakini hatima ya Bw Zida bado haijulikani.

Walinzi hao wa rais walimtangaza Jenerali Gilbert Diendere kuwa kiongozi wao.