Treni ya umeme yaanza kutumika Ethiopia

Treni Ethiopia Haki miliki ya picha AFP
Image caption Treni hiyo inatarajiwa kurahisisha usafiri na kupunguza msongamano wa magari Addis Ababa

Ethiopia imezindua rasmi usafiri za treni ya umeme ya kubeba abiria mijini, ambayo ndiyo ya kwanza katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Treni hiyo itatumika katika mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa kwenye reli ya umbali wa kilomita 34, ikipita mji huo kutoka kaskazini kwenda kusini.

Mradi huo umegharimu $470 milioni (£300 milioni, ukifadhiliwa kwa kiasi kikubwa na Uchina. Mamlaka nchini humo zimesema mradi huo, utafanyakazi kwa saa 16 na unatarajiwa kupunguza msongamano wa magari barabarani, huku watu milioni moja wakitarajiwa kuutumia kila siku.

Nauli inatarajiwa kuwa chini ya nusu dola kwa kila safari.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mradi huo ulifanikishwa kupitia ufadhili kutoka Uchina

Mwandishi wa BBC mjini humo Emmanuel Igunza, aliyehudhuria uzinduzi wa treni hiyo, anasema raia walijawa na msisimko mkubwa na kila mmoja alitaka kuwa wa kwanza kuiabiri.