Walinzi wa rais Burkina Faso ‘kupigana’

Burkina Demos
Image caption Wanajeshi wamelakiwa kwa shangwe na waandamanaji ambao wamekuwa wakipinga mapinduzi

Viongozi wa mapinduzi Burkina Faso wamekataa kutii makataa ya kusalimu amri na kutishia kupigana vita wakishambuliwa.

Walinzi wa rais walioongoza mapinduzi walikuwa wamepewa hadi saa nne saa za huko kuweka chini silaha na wanajeshi ambao walifika katika mji mkuu Ouagadougou usiku.

Hayo yamejiri huku marais wa mataifa ya Afrika Magharibi chini ya muungano wa Ecowas wakikusanyika Abuja, Nigeria kufahamishwa na Rais wa Senegal Macky Sall kuhusu hatua zilizopigwa katika kutatua mzozo huo.

Duru zinasema mashaurino ya kupatanisha wanajeshi hao na walinzi waliopindua serikali yaligonga mwamba usiku, suala tata likiwa hatima ya walinzi hao wa rais.

Rais Sall amekuwa akiongoza mashauriano akishirikiana na mwenzake wa Benin Yayi Boni.

Barabara za kuelekea ikulu ya rais hazina watu wala magari huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda Ouagadougou.

Kiongozi wa mapinduzi Jenerali Gilbert Diendere alikuwa awali ameambia BBC kwamba yuko tayari kurejesha mamlaka kwa uongozi wa kiraia, lakini baada tu ya mpango wake wa kumaliza mzozo wa sasa kuungwa mkono na viongozi wa mataifa ya eneo hilo.

Akiongea kutoka mafichoni, Jenerali Diendere aliambia BBC: “Kuwa tayari kusalimu amri? Hatujafika huko bado …Tungependa kuendelea na mazungumzo na tunawaambia wote kwamba tuko tayari kutekeleza maamuzi ya Ecowas (kundi la mataifa ya Afrika Magharibi).”

Aidha, aliomba radhi kwa raia, akisema hilo tu ndilo wawezalo kufanya kwa sasa.

Walinzi wa rais waliopindua serikali ni watiifu kwa kiongozi aliyetimuliwa mamlakani mwaka jana Blaise Compaore.

Walimzuilia Kaimu Rais Michel Kafando Jumatano iliyopita, na kumtangaza Jenerali Diendere kuwa kiongozi mpya.

Tangu wakati huo, watu 10 wameuawa kwenye makabiliano kati ya waandamanaji wanaopinga mapinduzi hayo na maafisa wa usalama. Watu zaidi ya 100 wamejeruhiwa.

Balozi wa Ufaransa nchini Burkina Faso, Gilles Thibault, aliandika kwenye Twitter kwamba Bw Kafando ameachiliwa huru na sasa yumo kwenye makao ya balozi huyo.