Mawaziri EU waafikiana kuhusu wahamiaji

Wahamaiaji Ujerumani Haki miliki ya picha Getty
Image caption Baadhi ya mataifa Ulaya yamekuwa yakipinga wazo la kushurutishwa kupokea wahamiaji

Mawaziri wa masuala ya ndani wa Muungano wa Ulaya wamekubaliana kuhusu mpango wa kuwapokea wahamiaji 120,000 walioingia katika bara Ulaya.

Mpango huo umeidhinishwa kwa kupata wingi wa kura.

Chini ya mpango huo, wahamiaji watasafirishwa kutoka Italia, Ugiriki na Hungary hadi nchi nyingine za EU.

Romania, Jamhuri ya Czech, Slovakia na Hungary zilipiga kura kupinga mpango huo wa kutengea kila nchi idadi ya wahamiaji inaofaa kupokea.

Lakini mataifa mengi ya muungano huo yameunga mkono mpango huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.

Finland ndiyo nchi pekee iliyosusia kura hiyo. Poland, iliyokuwa awali imepinga mpango huo, ilipiga kura kuuidhinisha.

Mwandishi wa BBC aliyeko Brussels Chris Morris amesema ni jambo nadra sana kwa suala kama hilo linalohusu uhuru wa mataifa kuamuliwa kwa kura ya wengi badala ya kauli ya pamoja.

Mpango huo sasa unatarajiwa kuidhinishwa na viongozi wa mataifa ya EU katika mkutano wa pili utakaofanyika Jumatano mjini Brussels.