Kiongozi wa seneti Nigeria afika kortini

Bukola Saraki
Image caption Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amekuwa mstari wa mbele kuhimiza uwazi miongoni mwa maafisa wa umma

Rais wa Bunge la Seneti nchini Nigeria, Bukola Saraki, amefika kortini Abuja leo ambako anakabiliwa na makosa 13 yanayohusu maadili.

Makosa hayo ni pamoja na kuhadaa akitangaza mali yake pamoja na kukosa kutangaza mkopo, makosa ambayo anayakanusha.

Alikuwa ametarajiwa kufika kortini mara mbili awali lakini hakufika.

Kesi dhidi yake inaendeshwa na jopo la mahakama kuhusu maadili na inahusu makosa anayodaiwa kuyatenda alipokuwa gavana wa jimbo la Kwara kati ya mwaka 2003 na 2011.

Jopo hilo lilikuwa limetoa kibali cha kukamatwa kwake Ijumaa wiki iliyopita baada yake kukosa kufika kortini.

Bw Saraki, amekuwa akijitetea na kushangaa ni kwa nini imechukua miaka 12 kutambua kwamba kulikuwa na kasoro katika karatasi zake za kutangaza mali yake na pesa anazodaiwa.