Rais Kafando arudi mamlakani Burkina Faso

Haki miliki ya picha
Image caption Rais wa mpito Michel Kafando

Rais wa mpito nchini Burkina Faso Michel Kafando amerejeshewa tena mamlaka katika hafla iliyofanyika mjini Ouagadougou takriban wiki moja baada ya mapinduzi.

Sherehe ya kumrejesha mamlakani ilihudhuriwa na viongozi kadha wa mataifa ya Magharibi ambao wamesaidia sana kwenye mashauriano.

Rais Kafando aliwashukuru sana viongozi hao, huku akishangiliwa na wanasiasa na viongozi wa mashirika ya kijamii.

Rais wa Benin Thomas Boni Yayi, mmoja wa walioongoza mashauriano hayo, alihudhuria sherehe hiyo na kusema sasa lazima juhudi zifanywe haraka kuhakikisha kunafanyika uchaguzi huru na wa haki.

Uchaguzi mkuu nchini humo ulikuwa umepangiwa kufanyika Oktoba 11.

Bado kuna utata kuhusu iwapo viongozi wa mapinduzi watasamehewa.

Walinzi wa rais waliokuwa wametwaa mamlaka wakiongozwa na jenerali Gilbert Diendere walikubali mkataba wa kuondoka mamlakani usiku wa kuamkia leo.

Waliahidi kurudi kambini huku jeshi la kawaida lililokuwa limewapa makataa ya kuweka chini silaha Jumanne likiondoka katika mji mkuu.

Walinzi hao wa rais ni watiifu kwa aliyekuwa rais wa taifa hilo Blaise Compaore ambaye aliliongoza taifa hilo kwa miaka mingi kabla ya kung'atuliwa mamlakani mwaka uliopita.