Walinzi wa rais Burkina Faso wasalimu amri

Vikosi vya Burkina Faso Haki miliki ya picha AFP
Image caption Hatua ya walinzi wa rais kukubali kuondoka uongozini imeondoa wasiwasi wa kuzuka vita

Walinzi wa rais waliopindua serikali nchini Burkina Faso wamekubali kurejesha madaraka kwa serikali ya kiraia na kurejea kwenye kambi zao.

Hatua hiyo imehitimisha mzozo uliokuwa umetokea baada ya wanajeshi watiifu kwa Rais Michel Kafando kuwasili mji mkuu na kuwataka walinzi hao wa rais waliopindua serikali kusalimu amri.

Mkataba kati ya viongozi hao wa mapinduzi na viongozi wa jeshi ulitiwa saini usiku, huku wapatanishi kutoka muungano wa mataifa ya Afrika Magharibi Ecowas wakitarajiwa kuwasili katika mji mkuu Ouagadougou leo.

Kwa mujibu wa kiongozi wa kabila la Mossi Bw Mogho Naaba, aliyenukuliwa na shirika la habari la Reuters, chini ya mkataba huo, walinzi hao wa rais wataondoka barabara za mji wa Ouagadougou na kurejea kambini huku nao wanajeshi wakiondoka mjini na kukaa kilomita 50 kutoka mji huo.

"Wanataka kuepusha mapigano kati ya wanajeshi hao … ndio wanaofaa kulinda watu na mali yao. Nawasihi kusameheana.

Walinzi wa rais, ambao walikuwa watiifu sana kwa rais aliyetimuliwa mamlakani Blaise Compaore, watakaa katika kambi Naba Koom II, ngome yao katika mji mkuu.

Lazima wahesabu silaha walizo nazo katika muda wa saa 72 zijazo.

Kufuatia mkutano mkuu wa dharura wa viongozi wa Ecowas nchini Nigeria Jumanne, marais wa Senegal, Togo, Benin,

Ghana, Niger na Nigeria walikuwa wamepangiwa kusafiri Burkina Faso leo kuhakikisha Michel Kafando anarejeshewa mamlaka.