Walioongeza bei ya dawa 5000% wabadili msimamo

Martin Shkreli
Image caption Shkreli hata hivyo ametetea kuongezwa kwa bei akisema kungesaidia utafiti wa dawa mpya

Kampuni ya kutengeneza dawa iliyoshutumiwa sana baada ya kuongeza bei ya dawa inayotumiwa na wanaougua Ukimwi kwa asilimia 5,000 imesema itapunguza bei hiyo.

Martin Shkreli, mkuu wa kampuni ya Turing Pharmaceuticals, ameambia vyombo vya habari Marekani kwamba bei hiyo itapunguzwa baada ya kilio kutoka kwa umma, lakini hakusema ni kwa kiwango gani.

Turing Pharmaceuticals ilinunua haki za kutengeneza dawa ya Daraprim mwezi Agosti.

Muda mfupi baadaye, iliongeza bei ya dawa hiyo, inayotumiwa kukabiliana na maambukizi, kutoka $13.50 (£8.70) hadi $750.

Licha ya shutuma kutoka hata kwa makundi ya matabibu, moja likitaja bei hiyo kuwa isiyo ya haki, Bw Shkreli alitetea nyongeza hiyo akisema faida itatumiwa katika utafiti wa kutengeneza dawa mpya.

Hakuna haja ya wasiwasi wanaoishi Afrika kwa sababu dawa ya Daraprim haijadhibitiwa na sheria ya haki ya ubunifu na watengenezaji dawa wako huru kuitengeneza kote duniani.

Dawa hiyo sulfadoxine pyrimethamine (SP) 50%, ambayo unaweza ukanunua dukani kama tiba ya malaria kote barani.

Utafiti uliofanywa 2003 Nigeria kuhusu SP ulionyesha aina kumi za dawa hiyo zilikuwa zikitumiwa lakini hakuna hata moja iliyotengenezewa Marekani.