Ukuaji wa kiuchumi wa Uchina kwa kina

Ukuaji wa kiuchumi Uchina umepelekea ukuaji mkubwa wa miji na kusababisha mamia ya mamilioni ya wafanyakazi kutoka mashambani na kuelekea mijini kutafuta kazi. Hii hapa ni simulizi ya mabadiliko haya makubwa kwa picha, michoro na video.

Kwa mujibu wa takwimu za UN, idadi ya miji iliyo na wakazi milioni moja na zaidi Uchina imeongezeka pakubwa kutoka 16 mwaka 1970 hadi 106 mwaka 2015. Huu ni ukuaji wa juu sana ukilinganisha na miji 45 Marekani, na miji 55 Ulaya.

Hitaji kubwa la saruji

Kuhamia mijini kwa Wachina wengi kumeambatana na ongezeko kubwa katika ujenzi. Uchina iliwezaje kujenga haraka hivi? Usiende mbali, kwa mfano hapa kuna jengo hili moja refu lililochukua siku 19 kulijenga.

Soma mengi zaidi kuhusu nyumba ndefu za makazi za Mwenyekiti Zhang Lakini ingawa nyumba zinajengwa, hii haina maana kwamba watu wanaishi humo. Kuna miji mingi mipya yenye nyumba na maduka yasiyo na watu, na kuifanya miji hiyo kupewa jina la utani "miji hewa".

Image caption Ukungu na moshi

Ukuaji wa kiuchumi wa Uchina umeathiri sana mazingira - viwango vya uchafuzi wa mazingira vikipanda, uchafuzi mwingi ukitokana na viwanda vya kuzalisha stima vinavyotumia makaa ya mawe na ambavyo hututegemewa sana na Uchina kukidhi mahitaji yake ya kawi. Moja ya kisa kibaya zaidi cha ukungu na moshi kilichotokea mjini Beijing mwaka 2013 kilinaswa na kamera za satelaiti za Nasa. Picha za satelaiti zilizopigwa kutoka juu ya Beijing zinaonyesha ukungu unaotanda juu ya mji huo ukifikia viwango vibaya kushinda Januari 2013, picha iliyo hapa kulia ikionyesha ukungu wa rangi ya kijivu na hudhurungi ukifunika sehemu nyingi za mji. Uchina inajaribu kupunguza uchafuzi wa mazingira na imefunga viwanda vingi vinavyochoma makaa ya mawe. Hata hivyo, ni miji minane pekee kati ya 74 mikubwa iliyopita kigezo cha msingi zaidi cha ubora wa hewa kufuatia uchunguzi wa serikali 2014, kwa mujibu wa wizara ya mazingira.

Katika ubalozi wa Marekani jijini Beijing, kwa mfano, kiwango cha ubora wa hewa kimetajwa kuwa hatari sana kwa afya kwa mujibu wa vigezo vya Marekani kwa muda mrefu - ingawa kwa jumla siku zenye hewa hatari zimekuwa zikipungua tangu 2008, ubalozi huo ulipoanza kukusanya takwimu. Uchina ilianza kutoa takwimu sawa za ubora wa hewa 2012. Inasema vikwazo vya utoaji gesi vilivyowekwa pamoja na kufungwa kwa viwanda vya makaa ya mawe vimesaidia kupunguza uchaguzi wa hewa 2015.

Image caption Kuendelea kutajirika

Chama cha Kikomunisti kilianza kutekeleza sera za kibepari sokoni 1978. Baada ya kufungulia milango uwekezaji kutoka nje miaka ya 1980, Uchina imekuwa moja ya watengenezaji bidhaa wakuu duniani, viwanda vikitumia gharama ya chini ya kuwapata wafanyakazi kujifaa. Uchumi wa Uchina ulikua kwa kiwango cha kadiri cha 10% kwa mwaka kwa miongo mitatu hadi kufikia 2010, ingawa baada ya hapo ukuaji ulipunguza kasi. Katika miaka ya majuzi, taifa hilo liliipita Japan na kuwa taifa lenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, ingawa kiwango cha mapato ya kila mwaka kwa kila raia kimebaki chini ya Marekani, Japan, Ujerumani na Uingereza.

Image caption Furaha likizoni

Ukuaji wa uchumi wa Uchina umeambatana na kuongezeka kwa pesa za matumizi - Uchina ikiwa na idadi kubwa zaidi duniani ya watalii wanaozuru nchi nyingine, wageni kutoka taifa hilo wakiongoza kwa kutumia pesa nyingi zaidi duniani, wakitumia $165bn wakiwa likizoni. Maeneo wanayozuru sana Wachina ni Hong Kong, Japan, Ufaransa, Korea Kusini, Marekani na Thailand.

Image caption Ulaji wa nguruwe

Nyama ya nguruwe imekuwa kipenzi cha wengi Uchina, lakini ilikuwa ikiliwa nyakati maalum pekee kutokana na kiwango cha chini cha mapato. Hali si hiyo tena. Huku mapato ya raia yakiongezeka, kiwango cha nyama ya nguruwe inayoliwa kimeongezeka pakubwa, na sasa Uchina hula nusu ya nguruwe wanaoliwa duniani.

Image caption Kuachwa nyuma

Licha ya kuongezeka kwa mapato ya watu binafsi, watu hawajafaidika kwa njia sawa - pengo kati ya pesa za matumizi kwa Wachina wanaoishi mashambani na wanaoishi mijini likipanuka sana tangu 1990.

Mfumo wa usajili wa familia nchini Uchina, ujulikanao kama "hukou", umezidisha pengo hili, kwa sababu huzuia wafanyakazi wahamiaji kupata huduma ya afya, nyumba na huduma nyingine muhimu katika miji waliyoajiriwa kufanya kazi. Ongezeko kubwa la watu wanaohamia mijini pia limeathiri sana watoto. Uchina kwa sasa ina watoto 61 milioni wanaoishi vijiji vya mashambani bila wazazi wao walioenda mijini kutafuta ajira.