WHO yasema watu wengi Ulaya ni wanene

Mtu mnene Haki miliki ya picha SPL
Image caption Viwango vya unywaji pombe na uvutaji sigara Ulaya viko juu

Watu wengi Ulaya ni wanene kupita kiasi, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Ripoti hiyo kwa jina European Health Report inasema 59% ya watu wanaoishi ulaya wana uzani uliozidi au ni wanene sana.

Shirika hilo limesema eneo la Ulaya lililochunguzwa, ambalo hujumuisha baadhi ya maeneo ya bara Asia, ndilo lililokuwa na viwango vya juu zaidi vya unywaji pombe na uvutaji sigara duniani.

Kutokana na hayo, maafisa wa WHO wameonya kuwa huenda vijana wa eneo hilo “wasiishi muda mrefu kama walivyoishi mababu zao”.

Ipto hiyo imesimu baadhi ya mataifa kwa kupunguza vifo kutokana na saratani, kisukari na maradhi ya moyo.

Hata hivyo, imeonya kuwa 30% ya watu eneo hilo bado wanavuta sigara, kiwango ambacho kinazidi maeneo mengine yote.

Mkurugenzi wa WHO anayesimamia Ulaya Zsuzsanna Jakab amesema: "Ripoti hii imeonyesha matumaini. Lakini bado kuna hatari iwapo uvutaji sigara na unywaji pombe utaendelea kwa viwango vya sasa. Hii inahusu sana vijana ambao huenda wasiishi muda mrefu kama mababu zao.”