Bendera ya Somalia yatia wanamuziki taabani

Bendera ya Somalia Haki miliki ya picha AFP
Image caption Nyota ya Somalia yenye ncha tano huashiria umoja wa Wasomali

Wanamuziki watano wamekamatwa Somaliland wakituhumiwa kupeperusha bendera ya Somalia walipokuwa wakitumbuiza katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mwandishi wa BBC Abdinoor Aden anasema wanamuziki hao wa bendi ya Horn Stars, walikamatwa katika mji mkuu wa Somaliland, Hargeisa, punde baada yao kuwasili kwa ndege kutoka Mogadishu.

Bendera ya Somalia huwa na nyota yenye ncha tano, ishara ya kuonyesha umoja wa Wasomali.

Somaliland ilijitenga kutoka kwa Somalia 1991, lakini haijatambuliwa na Muungano wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) kama taifa huru.

Wakazi wa Somaliland wamekuwa wakipigania kutambuliwa kwa taifa hilo na jamii ya kimataifa.

Naibu waziri wa masuala ya ndani Ahmed Cadarre ameambia redio ya BBC ya Kisomali kuwa wanamuziki hao wanazuiliwa kwa kutumbuzia katika tamasha za kupinga uhuru wa Somaliland, ilhali wanafanyia kazi wizara ya habari.

Makundi ya mashabiki mtandaoni wameingia kwenye Twitter na kuanzisha kitambulizi cha #freehornstars kupinga kukamatwa kwa wanamuziki hao na kuitisha kuachiliwa huru kwao.

Bendi hiyo ilitumbuiza wakati wa sherehe za Eid mjini Mogadishu.