Mourinho adai Diego Costa anaonewa

Diego Costa Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Costa alipigwa marufuku mechi tatu na Shirikisho la Soka la Uingereza

Meneja wa Chelsea Jose Mourinho amedai mshambuliaji wake Diego Costa amekuwa akionewa na maafisa wasimamizi wa soka.

Akiongea na wanahabari kuhusu mechi ya leo kati ya kilabu yake na Porto ya Ureno katika Ligi ya Kilabu Bingwa Ulaya, Mourinho alisema kuna hamu kubwa ya kumsimamisha au kumpiga marufuku mchezaji huyo miongoni mwa waamuzi.

Costa alipigwa marufuku mechi tatu na Shirikisho la Soka la Uingereza baada ya kupatikana na hatia ya utovu wa nidhamu wakati wa mechi dhidi ya Arsenal ligi kuu.

Lakini yuko huru kucheza dhidi ya Porto leo kwani marufuku hiyo haigusi mechi za Ulaya.

Alipoulizwa iwapo angelipenda kuwa na wachezaji 11 walio kama Costa uwanjani, Mourinho alisema: “Tungeshindwa kila mechi, kwa sababu hamu ya kumpiga marufuku iko juu mno kiasi kwamba tungekosa wachezaji wa kuanza nao mechi.”

“Nina furaha tu kwamba kwa sasa nina mmoja tu na mwache acheze hadi waamue kumpiga marufuku tena.”

Costa amekosa mechi mbili Uingereza, na pia atakosa mechi ya wikendi dhidi ya Southampton.

Kwenye kikao hicho na wanahabari, Mourinho pia alionya wachezaji wake kwamba hakuna aliye salama iwapo kilabu hiyo itaendelea kuandikisha matokeo mabaya.

Mourinho amekuwa akimuweka benchi John Terry mechi mbili zilizopita za Ligi ya Premia, ihali Branislav Ivanovic na Cesc Fabregas pia wamekosolewa kutokana na uchezaji wao.

"Watu wasioguswa, ni uendelevu pekee unaoweza kukupa hadhi hiyo,” alisema Mourinho, ambaye vijana wake wamo nambari 14 ligini baada ya mechi saba kucheza.