Urusi yasema huenda ikashambulia IS

Vladimir Putin Haki miliki ya picha EPA
Image caption Putin na Obama hawakuelewana kuhusu hatima ya Rais wa Syria Bashar al-Assad

Urusi imesema inatafakari uwezekano wake kufuata Marekani na kushambulia kwa ndege wapiganaji wa Islamic State (IS), Rais Vladimir Putin anasema.

Bw Putin amesema hayo baada ya kukutana na Barack Obama pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Lakini mkutano huo, na hotuba za viongozi hao UNGA, pia viliashiria mgawanyiko kuhusu jinsi ya kumaliza vita Syria.

Urusi ilisema itakwua “kosa kubwa” kutofanya kazi na Rais wa Syria Bashar al-Assad kukabiliana na IS.

Jumatatu, Marekani na Ufaransa zilisizitiza tena kwamba Rais Assad sharti aondoke mamlakani.

Lakini akijibu, Bw Putin alisema: “Hao si raia wa Syria na kwa hivyo hawafai kuhusika katika kuamua viongozi wa taifa jingine.”

Urusi ilisema itafanya tu mashambulio ya ndege iwapo hilo litaidhinishwa na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo alifutilia mbali uwezekano wa wanajeshi wa Urusi kushiriki operesheni ya kijeshi ya ardhini Syria.

Putin na Obama walikutana dakika 90 kwa mazungumzo ambayo Putin alisema yalikuwa ya uwazi nay a kufana.

Ilikuwa mara ya kwanza kwao kukutana ana kwa ana katika kipindi cha mwaka mmoja.