Juma Said apigwa marufuku ya miaka 2

Image caption Juma Said apigwa marufuku ya miaka 2

Nahodha wa klabu ya Tanzania ya Mbeya City, Juma Said maarufu ‘Nyosso’ amepigwa marufuku ya kutocheza kwa muda wa miaka miwili baada ya kamati inayosimamia ligi kuu ya Tanzania kupokea ripoti ya mechi za ligi hiyo zilizochezwa na kumpata na hatia ya utovu wa nidhamu.

Mchezaji huyo pia ametozwa faini ya shilingi milioni mbili ya Tanzania (2,000,000) kwa kitendo kinachokiuka nidhamu za soka ikiwemo kumdhalilisha mchezaji wa mabingwa wa kombe la CECAFA mwaka huu, Azam FC, John Bocco.

Nahodha huyo wa Mbeya, alishiriki katika kitendo hicho katika mchuano wa ligi kati ya timu yake na Azam ulioandaliwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Kufikia sasa timu yake ya Mbeya city, haijatoa taarifa kuhusu uamuzi wa bodi hiyo.

Hata hivyo, kwenye taarifa kwa umma, Mbeya Fc imesema kuwa katibu wake mkuu ameiagiza idara ya mawasiliano na mahusiano ya klabu kulichunguza tukio hilo kwa kutazama rejea na mazingira iliyopelekea tukio hilo.

Mchezaji huyo pia anatarajiwa kukutana na bodi hiyo kwa uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.

Mbeya FC imepeana makataa ya saa 86 kuanzia jana ili kukamilisha uchunguzi na akuwasilisha ripoti kamili.

Mapema mwaka huu mchezaji huyo alihudumia marufuku ya mechi nane kwa kufanya tendo kama hilo.