Buhari awataka raia Nigeria waache utundu

Muhammadu Buhari
Image caption Buhari amesema sharti raia Nigeria wakubali kubadilika

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amewahimiza raia wa nchi hiyo waache “tabia ya utundu” ndipo taifa hilo liweze kustawi.

"Ili kuleta mabadiliko, lazima tubadilike na kuwa raia wanaotii sheria,” alisema akihutubu wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 55 tangu uhuru wa taifa hilo.

Bw Buhari alikuwa kiongozi wa kijeshi 1984 na 1985, na aliagiza wafanyakazi wa serikali waliochelewa kazini kuruka juu kama vyura, akijaribu kusisitiza nidhamu.

Alirejea uongozini Mei baada ya kushinda uchaguzi.

Nigeria ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi Afrika, na pia ndiyo huzalisha mafuta kwa wingi zaidi barani.

Hata hivyo, wengi wa raia wake huishi maisha ya umaskini, na taifa hilo hukumbwa na uhaba wa mafuta na umeme kupotea mara kwa mara.

"Mabadiliko hayafanyiki hivyo tu,” Buhari alisema akihutubia taifa hilo mara ya kwanza kabisa tangu aingie mamlakani.

“Lazima tubadilishe tabia yetu ya utundu katika shule, hospitali, sokoni, maegesho ya magari, barabarani, nyumbani na afisini,” akaongeza.

Hakutoa maelezo yoyote kuhusu ni sera gani ataanzisha kubadili tabia ya wananchi.

Miaka ya 1980, pamoja na kuaibisha wafanyakazi wa serikali wasiokuwa na nidhamu, pia alituma wanajeshi kulazimisha watu kupiga foleni wakisubiri magari ya uchukuzi wa umma.

Nigeria ina watu zaidi ya 166 milioni.

Bw Buhari, aliyesema majuzi kwamba atakuwa waziri wa mafuta, pia ametetea vikali hatua yake ya kushindwa kuteua baraza la mawaziri miezi minne baada ya kuchukua hatamu, akisema hataki kufanya uteuzi huo bila kumakinika.

"Lakini msijali, hamtasubiri zaidi. Kundi la kwanza la majina limetumwa kwa seneti,” alisema.

Majina hayo hayajatolewa hadharani.