Mbwa atumia wiki tatu kujifunza lugha mpya

Ginger Haki miliki ya picha PA
Image caption Mbwa huyo kwa jina Ginger anafuata maagizo kwa lugha ya Gaelic

Mbwa aliyekuwa akiandamana na mmiliki wake kwenye darasa la kujifundisha lugha ameshangaza wengi baada ya kuanza kuelewa lugha hiyo baada ya wiki tatu pekee.

Neil Smith alikuwa akiandamana na mbwa wake mwenye umri wa miaka mine kwa jina Ginger akienda kujifunza lugha ya Gaelic katika kanisa moja karibu na mji wa Dunoon.

Anasema alishangaa kuona jinsi mbwa huyo aina ya English Cocker Spaniel alianza kufuata maagizo yaliyotolewa kwa lugha hiyo kama vile keti (suidh), kaa (fuirich), njoo hapa (trobhad) na mbwa mzuri (cu math).

Mwalimu Elma McArthur alisema Ginger ni mbwa mwerevu sana.

Bw Smith na Ginger wamekuwa wakihudhuria darasa hilo katika kanisa la Strone Church of Scotland kila wiki pamoja na watu wengine 23.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Smith anasema anafurahia sana kuwa na mbwa anayefahamu lugha mbili

Mzee huyo wa miaka 67 alimsifu mbwa huyo wake anayemsaidia kusikia akisema imemuwezesha kujiamini zaidi.

“Nilikuwa mtu mwenye kuona hay asana na nilijihisi kutengwa hata nikiwa kwenye kundi la watu, au hata familia na marafiki,” amesema.

Anasema sasa anafurahia kujionyesha kwa watu wengine na kujivunia kwamba ana mbwa anayefahamu lugha mbili.