Michelle Obama ahimiza wasichana wasiogope wavulana

Michelle Obama Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bi Obama amekuwa akitetea sana elimu ya wasichana

Mke wa Rais wa Marekani Michelle Obama amewashauri wasichana waliobalege kutoogopa kupania kuwa “mtoto mwerevu zaidi darasani”.

Alisema wasichana hawafai kujali wavulana wanasema nini.

“Shindaneni na wavulana. Hakikisheni mmewashinda,” aliambia wasichana 1,000 wa shule pamoja na wanawake vijana alipokuwa akihutubu wakati wa hafla ya kupigia debe kampeni yake ya “Let Girls Learn” (Waacheni Wasichana Wasome). Lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha wasichana katika mataifa yanayoendelea wanapata elimu.

Aidha, inalenga kuwahimiza wasichana nchini Marekani kutumia nafasi zilizopo.

Bi Obama pia alitoa ushauri kwa wasichana waliobalehe jinsi ya kuepukana na presha za kubalehe.

“Najua kuwa tineja ni jambo ngumu lakini ni jambo la muda na si kovu litakalodumu maishani. Nusu ya watu hawa hutakutana nao utakapokuwa ukitimiza umri wa miaka 60,” alisema.

Kadhalika, aliwaambia kuwa kutia bidii masomoni hakuwezi kumfanya mtu kutofurahia maisha ya nje ya shule.

“Hakuna mvulana, katika umri huu wenu, ambaye ni mtanashati vya kutosha au wa kupendeza kiasi kwamba anaweza kukuzuia kupata elimu,” aliwaambia.

Bi Obama amekuwa akipigania sana elimu ya wasichana, hasa muhula wa pili wa utawala wa mumewe.

Alizidisha juhudi hizi baada ya wapiganaji wa Boko Haram kuteka nyara wasichana 200 nchini Nigeria Aprili 2014.

Firdaws Roufai, 15, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Central Park East jiji la New York, alimsifu mke huyo wa rais kwa kukiri kwamba utineja unaweza ukawa na changamoto nyingi.

“Hili limenipa motisha kuendelea kujikakamua,” anasema.