Bendera ya Palestina yaanza kupepea UN

Abbas Haki miliki ya picha AFP
Image caption Abbas amedai Israel imekuwa ikikiuka mikataba

Bendera ya Palestina imepeperushwa kwa mara ya kwanza katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.

Bendera hiyo ilipandishwa kwenye mlingoti kwenye sherehe iliyohudhuriwa na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.

Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw Abbas alisema ni jambo lisiloeleweka kwamba hadi sasa suala ya Palestina kuwa taifa bado halijatatuliwa.

Alionya kuwa Mamlaka ya Palestina anayoiongoza haijihisi tena kufungwa na mikataba kati yake na Israel kwa sababu mikataba hiyo hukiukwa mara kwa mara.

"Israel wanapoendelea kukataa kusitisha kuwajengea makao walowezi na kukataa kuachilia huru kundi la nne la wafungwa wa Kipalestina kwa mujibu wa makubaliano, hatuna budi ila kusisitiza kwamba hatutaendelea kujitolea katika utekelezwaji wa mikataba hii,” Bw Abbas amesema.

“Kwa hivyo tunatangaza kwamba hatuwezi kuendelea kufungwa na mikataba hii na kwamba Israel sharti ichukue majukumu yake yote kama taifa linalokalia nchi nyingine.”

Image caption Viongozi wa Palestina wanataka eneo hilo litambuliwe kama taifa

Afisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema hotuba ya Abbas ilikuwa ya “kijeuri” na “uchochezi na inahimiza kutoheshimiwa kwa sharia Mashariki ya Kati”.

"Tunatarajia viongozi wa Mamlaka (ya Palestina) na viongozi wake kuwajibika na kukubali pendekezo la … Israel na kuingia kwenye mazungumzo na Israel bila masharti yoyote.”

Mara kwa mara, Bw Abbas amekuwa akitishia kuvunja Mamlaka ya Palestina na kukabidhi jukumu la kusimamia Ukingo wa Magharibi kwa Israel iwapo hakutakuwa na matumaini ya kupatikana kwa mkataba wa Amani.