Wanawake wa kujitoa mhanga washambulia Maiduguri

Boko Haram Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Buhari aliahidi kukabiliana vilivyo na wapiganaji wa Boko Haram akichaguliwa kuongoza Nigeria

Kundi la wanawake wa kujitoa mhanga limetekeleza mashambulio kadha ya mabomu katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Idadi ya waliofariki bado haijabainika lakini jeshi la Nigeria linasema watu 14, wakiwemo wanawake hao wa kujitoa mhanga, wamefariki na wengine 39 kujeruhiwa.

Mashambulio hayo yalitekelezwa Alhamisi jioni na yalilenga misikiti, watu walipokuwa wamekusanyika kwa sala ya jioni.

Aidha, walishambulia nyumba ya kiongozi mmoja wa kundi la kujilinda la wakazi.

Mashambulio sawia na hayo wiki mbili zilizopita karibu na eneo lililoshambuliwa yaliua zaidi ya watu 100.

Kundi la Kiislamu la Boko Haram limekuwa likidaiwa kuhusika katika mashambulio hayo ya kujitoa mhanga.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari aliahidi kukabiliana na wapiganaji hao, na jana alikuwa akiongoza taifa hilo kuadhimisha miaka 55 tangu kujinyakulia uhuru.