Walimu wasitisha mgomo Kenya

Image caption Katibu mkuu wa chama cha walimu nchini KNUT Wilson Sossion

Mgomo wa walimu nchini Kenya hatimaye umesitishwa.

Walimu sasa watarudi shuleni ili kuendelea kufunza siku ya jumatatu.

Katibu mkuu wa KNUT Wilson Sossion amesema kuwa muungano huo hatahivyo hautaondoa kesi ambapo tume ya huduma za walimu TSC imekataa rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama wa kuwapatia walimu hao nyongeza ya mishahara ya kati ya asilimi 50-60

Hatua hiyo ya muungango wa walimu nchini Kenya KNUT inatokana na agizo lililotolewa na Jaji Abuodha mnamo tarehe 25 mwezi Septemba.

Mgomo huo ulikwamisha masomo nchini Kenya huku walimu wakitaka nyongeza ya mishahara pamoja na ile ya marupurupu.

Walimu sasa wanaitaka tume ya kuajiri walimu TSC kuwapatia mishahara ya mwezi Septemba baada ya tume hiyo kusema kuwa haitawalipa kwa kuwa walikuwa katika mgomo.

Hatua hiyo inatoa afueni kwa wanafunzi wa shule za uma ambao walilazimika kukaa nyumbani kwa kipindi chote cha mgomo huo.

Image caption Walimu

Jaji wa mahakama ya wafanyikazi Nelson Abuodha aliwaagiza miungano yote miwili ya walimu kuahirisha mgomo huo ili kutoa fursa ya majadiliano.

''Kwa maslahi ya watoto wetu katika shule za umma na haki zao chini ya katiba mpya,mahakama imeagiza miungano hiyo ya walimu kuahirisha mgomo huo ulioanza terehe mosi mwezi Septemba kwa siku 90,ili wanachama wake waanza kazi mara moja'',alisema jaji Abuodha.

Mda mfupi tu baada ya agizo hilo kutolewaserikali ilitangaza kuwa shule zote zitafunguliwa sikuya jumatatu na kufungwa mnamo tarehe 20 mwezi Novemba