Burundi yamfukuza mwanabalozi wa Rwanda

Nkurunziza Haki miliki ya picha
Image caption Mataifa haya mawili yamekuwa yakilaumiana siku za hivi karibuni

Serikali ya Burundi imemfurusha afisa wa ubalozi wa Rwanda nchini humo kwa madai kwamba amekuwa akihusika katika kuhujumu usalama nchini humo.

Balozi wa Rwanda nchini Burundi amethibitisha kufukuzwa kwa Bw Desire Nyaruhirira.

Uhusiano kati ya Rwanda na Burundi umekuwa ukidorora hasa tangu kutekelezwa kwa jaribio la kumpindua Rais Pierre Nkurunziza.

Majuzi, Burundi ilidai Rwanda imekuwa ikiwafunza na kuwasaidia waasi wanaotaka kuvuruga hali ya usalama nchini humo.

Waziri wa masuala ya kigeni wa Burundi Alain Nyamitwe pia aliambia BBC kwamba Rwanda inamhifadhi kiongozi wa jaribio la mapinduzi yaliotibuka mbali na kuwasaidia waasi kutekeleza mashambulizi mipakani, ameiambia BBC.

Rwanda imekana madai hayo na kusema Burundi inajaribu kupotosha watu kuhusu matatizo yake.