Utafiti: Kompyuta na simu zinadhoofisha bongo

Tarakilishi Haki miliki ya picha Science Photo Library
Image caption Watu wengi siku hizi hukimbilia tarakilishi na simu kutafuta habari badala ya kutumia akili

Tabia ya kutegemea sana kompyuta na programu za kusaka habari mtandaoni inawafanya watu kupoteza uwezo wa kukumbuka mambo, utafiti mpya unaonyesha.

Utafiti huo umeonyesha sasa watu wanatumia sana tarakilishi badala ya kuweka habari akilini.

Watu wengi wazima ambao waliweza kukumbuka nambari za simu walizokuwa wakitumia utotobi sasa hawawezi kukumbuka moja kwa moja nambari za simu wanazotumia kazini au hata nambari za simu za jamaa na marafiki.

Maria Wimber kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham anasema mtindo wa kuangalia kila kitu kwenye kompyuta au simu “unazuia kukua kwa sehemu ya ubongo inayohifadhi habari kwa muda mrefu”.

Utafiti huo ulichunguza tabia ya uhifadhi habari ya watu wazima 6,000 katika mataifa ya Uingereza, Ufaransa, Italia, Ujerumani, Uhispania, Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg.

Watafiti waligundua zaidi ya thuluthi moja ya walioshiriki walikimbilia kompyuta walipotaka kutafuta habari fulani.

Uingereza iliongoza, huku zaidi ya nusu “wakichakura mtandaoni kwanza kutafuta jibu”.

Walioongoza utafiti huo wanasema kutegemea sana kompyuta kunaweza kuwa na madhara ya kudumu kwa sehemu inayohifadhi mambo muda mrefu kwenye ubongo.

Hii ni kwa sababu habari zinazopatikana kwa urahisi kwenye mitambo ya kiteknolojia zinaweza kusahaulika upesi.

"Ubongo wetu huwa unaimarika katika kukumbuka jambo kila tunapoutumia kulikumbuka, na huwa tunasahau mambo tusiyotumia sana ambayo huonekana kusumbua akili,” alisema Dkt Wimber.

Haki miliki ya picha CGNet Swara
Image caption Simu zimekuwa kama sehemu ya mwili wa watu

Anasema kutumia ubongo kukumbuka jambo ni njia nzuri sana ya kumfanya mtu asisahau jambo au habari hizo.

Miongoni mwa watu wazima wa Uingereza walioshirikishwa, 45% walikumbuka nambari ya simu waliyotumia nyumbani walipokuwa watoto wa umri wa miaka 10, na 29% walikumbuka nambari zao binafsi walizotumia wakiwa watoto. Asilimia 43 walikumbuka nambari za kazini.

Uingereza ilishika mkia kwa watu walioweza kukumbuka nambari za simu za wachumba wao kwenye utafiti huo Ulaya. Ni asilimia 51 pekee waliozikumbuka namba hizo kwa kichwa. Italia iliongoza ikiwa na asilimia 51.