Wasifu wa Seif Sharif Hamad

Image caption Maalim Seif amezaliwa katika kijiji cha Nyali, kisiwani Pemba mnamo tarehe 22 mwezi wa Oktoba mwaka 1943.

Maalim Seif Sharif Hamad, sio mgeni katika masikio ya watu hasa katika siasa za Zanzibar na Tanzania bara kwa ujumla.

Hivi sasa yeye ni makamu wa kwanza wa rais wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar na pia ni katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF au Civic United Front.

Yeye ndie anaepeperusha bendera ya urais wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar.

Maalim Seif amezaliwa katika kijiji cha Nyali, kisiwani Pemba mnamo Oktoba 22, 1943.

Kutokana na mazingira magumu ya miaka hiyo, na shule kuwa mbali na alipokuwa anaishi, Maalim alikuwa na kibarua cha kuvuka bahari kila siku kwa kutumia mtumbwi kwenda na kurudi shule.

Nyota ya kusiasa ya Maalimu Seif inaonekana kuanza kugara punde tu baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kurudi nyumbani.

Image caption Ni makamu wa kwanza wa rais wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar na pia ni katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF au Civic United Front.

Aliteuliwa kuwa msaidizi maalumu wa aliyekuwa rais wa Zanzibar Aboud Jumbe.

Muda mfupi baada ya uteuzi huo, Maalimu Seif aliteuliwa kuwa waziri wa elimu Zanzibar, baada ya Baraza la mawaziri kuvunjwa.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo, nafasi ya uwaziri wa elimu na utamaduni, ndio iliyompa fursa ya kisiasa Maalim kuanza kuwatumikia wanzazibari.

Baada ya hapo, Maalim ameweza kushika nyadhifa mbali mbali kwa nyakati tofauti, ikiwemo nafasi ya waziri kiongozi ambayo ni sawa na nafasi ya waziri mkuu.

Hata hivyo, hakuna siasa isiyokuwa na milima na mabonde. Mwaka 1988, Maalim Seif aliondolewa katika baraza la mawaziri na hatimae kutimuliwa ndani ya chama cha CCM.

Tofauti za kimsimamo ndani ya chama ndicho kilicho kuwa chanzo kikubwa cha yeye na wenzake kufukuzwa.

Image caption Mwaka 2010, alipoingia katika kinyang'anyiro cha urais na rais wa sasa wa Zanzibar Dk.Ali Mohammed Shein

Hata hivyo, vuguvugu hiyo aliyoianzisha ndio iliyozaa chama cha wananchi CUF ambapo alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kwanza, nafasi aliyoihudumia mpaka mwaka 1999 ndipo alipochaguliwa kuwa katibu mkuu hadi hivi sasa.

Maalim Seif ameshiriki katika mbio za urais za Zanzibar mara nne mfululizo bila mafanikio.

Ingawa matokeo ya chaguzi hizo yanadaiwa kugubikwa na utata huku baadhi ya wafuasi wake wakidai kwamba Maalim ameibiwa kura.

Baadhi ya nyakati, Maalimu alilazimika kutumia hekima na busara zake, na ukomavu wake wa kisiasa kuwatuliza wafuasi wake.

Mwaka 2010, alipoingia katika kinyang'anyiro cha urais na rais wa sasa wa Zanzibar Dk.Ali Mohammed Shein, katika hotuba yake, Maalimu Seif, kwa shingo upande, alikubali matokeo, lakini pia aliitaka tume ya uchaguzi Zanzibar kuyafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza.

Image caption Moja wapo ya sifa zake kuu ni ile ya kuwa na msimamo ambao hautetereki

Maalim ni miongoni mwa wanasiasa ambao wanaonekana kuwa na nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Moja wapo ya sifa zake kuu ni ile ya kuwa na msimamo ambao hautetereki hasa katika suala la kudai mamlaka kamili ya Zanzibar.

Wakati huo huo, baadhi ya wanasiasa hasa wale ambao wamewahi kukwaruzana na Maalim, wanahisi kwamba, sio sahihi kwa Maalim kubaki katika uongozi wa chama hicho kwa muda mrefu bila kupisha wengine.