Fundi stadi asiyeona aliyemshonea Kikwete shati

Abdallah Nyangalio
Image caption Nyangalio haoni lakini ni fundi stadi

Ni kawaida kuwapata mafundi wa nguo wakitumia utepe wa kupimia kuwapima wateja wao kabla ya kuwashonea nguo.

Lakini ukikutana na Abdallah Nyangalio, fundi hodari nchini Tanzania, mara nyingi hutampata akitumia utepe.

Kwa kukugusa tu, atakuwa tayari amejua vipimo vya nguo inayokufaa, ingawa hali ikizidi hutumia utepe maalum alioukarabati ndipo kupata vipimo kwa ufasaha.

Alianza kufanya hivi baada yake kupoteza uwezo wa kuona 1989, katika hali ya kusikitisha.

Alipatwa na maumivu makali ya kichwa 1988 na akawa anatafuta tiba bila mafanikio.

Mwaka 1989, alikutana na daktari kutoka Urusi aliyeahidi kumtibu na akamfanyia upasuaji.

Lakini badala ya kumpona, alipofuka kabisa na mke wake alimtoroka..

Image caption Hizi hapa ni baadhi ya nguo alizoshona

Hata hivyo, daktari huyo hakumuacha mikono mitupu.

Daktari huyo alimfunza jinsi ya kushona nguo kwa miezi mitatu na tangu wakati huo, hajarudi nyuma.

Mwandishi wa BBC Swahili Esther Namuhisa, alimtembelea katika duka lake jijini Dar es Salaam leo ikiwa siku ya kuona duniani.

Fundi huyo wa miaka 52 ameibuka maarufu kiasi kwamba hata amemshonea shati Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete.

Licha ya hili, bado anaikosoa serikali kwa kutotambua vipaji vya walemavu, anaosema wengi wao huishia kuwa ombaomba barabarani.

Kitu pekee anachohitaji kusaidiwa ni katika kuchagua rangi, lakini kazi hiyo nyingine atajifanyia mwenyewe.

Image caption Hapa, Bw Nyangalio alikutana na Rais Kikwete maonyesho ya biashara ya kimataifa ya Sabasaba, Dar es Salaam

Alifanikiwa kumpata mke mwingine na hana huzuni tena kutokana na hali kwamba haoni.

Ingawa yeye hutembea kwa kutumia kijiti, huwa ana uwezo wa kumtambua mtu hata kabla ya mtu kutamka neno.

Huwa anaweza kuendesha pikipiki na ni kiongozi wa wahudumu wa bodaboda na bajaji eneo la Temeke.