Mawaziri wa Nato wakutana kujadili Urusi

Ndege ya Urusi Haki miliki ya picha AP
Image caption Urusi imesema ndege zake zinashambulia ngome za wapiganaji wa Islamic State

Mawaziri wa ulinzi wa mataifa wanachama wa muungano wa kujihami wa Nato wanakutana leo kujadili mashambulio yanayotekelezwa na Urusi nchini Syria.

Mkutano huo utakaofanyika mjini Brussels unafanyika baada ya mmoja wa wanachama wa Nato Uturuki kusema ndege za kijeshi za Urusi ziliingia anga yake.

Urusi imefyatua mizinga kutoka manowari yake pamoja na kutekeleza mashambulizi kutoka angani kumsaidia kiongozi wa Syria Bashar al-Assad.

Lakini Moscow imekanusha matai ya nchi za Magharibi kwamba mashambulio hayo yanawalenga wapinzani wa Assad, baadhi wanaosaidiwa na mataifa ya Magharibi, na wala si wapiganaji wa kundi la Islamic State (IS).

Mwandishi wa BBC anayeangazia masuala ya ulinzi Jonathan Marcus amesema Nato inadhamiria kueleza wazi kwamba itajibu mashambulio yoyote.

Alhamisi, Katibu Mkuu wa Nato Jens Stoltenberg alisema muungano huo ulieleza kutofurahishwa kwake na kuongezeka kwa “uwepo wa kijeshi” wa Urusi nchini Syria.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Stoltenberg ameitaka Urusi kutomuunga mkono Bashar al-Assad

Aliitaka Moscow kuonyesha ushirikiano katika kukabiliana na IS na kukoma kumuunga mkono Bw Assad.

Lakini aliongeza kuwa hali ya sasa inahitaji inaonyesha hitaji la kutatua mzozo wa Syria kisiasa.

Mawaziri hao wa Nato wanatarajiwa kutangaza uungaji mkono wao kwa Uturuki.

Aidha, wataangazia wasiwasi miongoni mwa mataifa wanachama wake eneo la Baltic kuhusu kuhusika kwa Urusi mashariki mwa Ukraine.

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Michael Fallon anatarajiwa kutangaza kwamba Uingereza iko tayari kutuma wanajeshi katika mataifa hayo ya Baltic.

Mnamo Jumatano, Urusi ilisema ilirusha makombora dhidi ya IS kutoka manowari zake zilizoko Bahari ya Caspian, takriban kilomita 1,500 kutoka Syria.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi pia alisema Moscow iko tayari kuwasiliana na kundi la waasi la Free Syrian Army linaloungwa mkono na nchi za Magharibi, kujadili jinsi ya kukabiliana na IS “na makundi mengine ya kigaidi”.

Lakini Waziri wa Ulinzi wa Marekani Ash Carter alisema majeshi ya muungano yanayopigana na IS nchini Syria hayatashirikiana na Urusi.