Tathmini:Maswala 5 makuu katika uchaguzi Tanzania

Image caption Maswala matano makuu katika Uchaguzi mkuu Tanzania

Yapo maswala mengi ambayo wapiga kura na wananchi kwa ujumla wanayatilia maanani kama vigezo vya kuwapigia kura wagombea katika uchaguzi huu.

Mnamo tarehe 25 Oktoba 2015, Tanzania itakuwa na uchaguzi mkuu ambao utahusishwa uchaguzi wa madiwani, wabunge na rais

Image caption Tathmini:Maswala 5 makuu katika uchaguzi Tanzania

Kwa mujibu wa ofisi ya taifa ya takwimu, zaidi ya wapiga kura Milioni 24 (24,252,927) watashiriki katika uchaguzi huu, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi inasema ni watu Milioni 23.7 ndio waliojiandikisha kupiga kura

Huu ni uchaguzi wa tano tangu Tanzania ianze siasa za vyama vingi, ambapo chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikishinda chaguzi zote nne zilizopita

Mwaka huu Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi ikiwa na vyama vya siasa 22, huku vyama vinne vikiwa vimeongezeka tangu uchaguzi mkuu uliopita

Image caption Mgombea wa chama tawala Chama Cha Mapiunduzi (CCM) John Magufuli amesema akichaguliwa kuingia madarakani ataanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kushughulika na ufasadi

Kuna jumla ya majimbo 264 Tanzania nzima ambayo yatahusishwa katika uchaguzi wa mwaka huu, huku visiwa vya Zanzibar vikiwa na majimbo 50

Kuna jumla ya wagombea urais wanane, huku wagombea ubunge wakiwa 1218 katika majimbo 264 na wagombea udiwani 10,897 katika kata 3,957

Kutakuwa na jumla ya vituo vya kupigia kura 72,000

Maswala ya Msingi

Kwa chaguzi nyingi zilizopita, suala la uchumi lilikuwa likipewa kipaumbele kabisa, lakini kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na asasi isiyo ya kiserikali Twaweza (ambao ulizua mjadala mkali nchini Tanzania), ni ajabu kwamba suala la uchumi limepelekwa mbele katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu

Kwa mujibu wa utafiti huo, ni maswala ya afya, maji na elimu, ndio ambayo yanaonekana kutiliwa maanani zaidi katika uchaguzi huu

Afya:

Hali ya huduma ya afya katika maeneo mengi nchini, hasa maeneo ya vijijini, bado ni mbaya sana.

Wananchi wengi bado wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za afya, na hata wanapofika katika vituo hivyo, hawapati huduma zenye kiwango kinachotakiwa.

Haki miliki ya picha PSCU
Image caption Zaidi ya wapiga kura Milioni 24 (24,252,927) watashiriki uchaguzi huu

Kuna uhaba mkubwa wa dawa muhimu, uchache wa vitanda hata katika hospitali nyingi mgonjwa zaidi ya mmoja wanalazimika kulala katika kitanda kimoja

Wananchi walipoulizwa juu ya vipaumbele vyao katika uchaguzi huu, wengi waliweka afya moja ya vipaumbele vikubwa vitatu

Elimu:

Japo kuwa Tanzania imesifiwa sana miaka ya hivi karibuni kwa juhudi zake katika sekta ya elimu, bado kuna mapungufu mengi katika sekta hii.

Kwa mfano, wakati takribani asilimia 94 ya watoto wenye umri wa kuandikishwa

darasala la kwanza, wamepelekwa shuleni, madarasa mengi yamefurika na wanafunzi kiasi kwamba wengi wanakaa chini na waalimu kuwa na wakati mgumu wa kufundisha idadi kubwa ya wanafunzi.

Kwa upande mwingine, hali ya kujifunza kwa wanafunzi hasa katika shule za msingi bado ni mbaya, kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni, ni asilimia 30 tu ya wanafunzi wa darasa la 3 wenye uwezo wa kufanya mazoezi ya

masomo ya Kiingereza, Kiswahili na Hisabati, huku karibu asilimia 30 ya wanafunzi wa darasa la saba hawawezi kusoma wala kukokotoa mazoezi ya hisabati ya darasa la 2.

Image caption Edward Lowassa, amesema ikiwa atachaguliwa ndani ya siku 100 atakuwa tayari ameshughulika na rushwa

Wapiga kura wengi katika uchaguzi huu wanataka kuskia wagombea wanamikakati gani katika kukabiliana na uduni huu katika sekta ya elimu

Maji:

Asilimia 30 ya Watanzania, yaani katika kila watu watatu, mtu mmoja anasema maji ni moja ya matatizo makubwa matatu yanayoikabili nchi.

Image caption Asilimia 30 ya Watanzania, yaani katika kila watu watatu, mtu mmoja anasema maji ni moja ya matatizo makubwa matatu yanayoikabili nchi.

Watanzania trakribani asilimia 89 wanapata maji kupitia vyanzo vya umma, kama vile visima vya umma.

Kwa maana nyingine ni mtu mmoja tu kati ya kumi (asilimia 11) ndio ana bomba au maji yamemfikia hadi nyumbani kwake

Rushwa:

Mgombea wa chama tawala Chama Cha Mapiunduzi (CCM) John Magufuli amesema akichaguliwa kuingia madarakani ataanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kushughulika na ufasadi na mafisadi pekee.

Kwa upande wake mgombea urais wa mwamvuli wa vyama vya upinzani (UKAWA) kupitia chama kikuu cha upinzani CHADEMA, Edward Lowassa, amesema ikiwa atachaguliwa ndani ya siku 100 atakuwa tayari ameshughulika na rushwa nchini. Kimsingi ahadi zote hizi zinavutia masikio mwa wapiga kura, lakini bila shaka Watanzania wanasubiri kuona ni kwa jinsi gani zitatekelezwa

Uchumi:

Image caption Takribani asilimia 40 ya wananchi wake (watu wazima) wanaingiza chini ya dola moja kwa siku

Wakati ukuwaji wa uchumi wa Tanzania unabashiri kwamba nchi hiyo itakuwa ya kipato cha kati hivi karibuni, takribani asilimia 40 ya wananchi wake (watu wazima) wanaingiza chini ya dola moja kwa siku, wakati tisa ya kumi ya Watanzania wote wanaingiza chini ya dola 3 kwa siku, wanasema World Bank.

Cha ajabu wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi utafiti wa hivi karibuni umeonesha wananchi hawaoni kama uchumi ni kipaumbele chao ukilinganisha na maji, afya na elimu.