Wapatanishi wa Tunisia wapewa tuzo ya Nobel

Image caption Wapatanishi

Mashirika manne yaliyopatanisha mzozo wa kisiasa nchini Tunisia yametunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka huu kwa mchango wake katika kufanikisha demokrasia nchini humo.

Akitangaza mshindi wa tuzo hiyo kuu, mwenyekiti wa kamati ya Nobel amesema kuwa kundi hilo la mashirika lilitoa mchango mkubwa katika kukuza demokrasia baada ya maandamano ya mwaka 2011.

Mashirika hayo manne ni muungano wa vyama vya wafanyakazi Tunisia (UGTT), shirikisho la viwanda, biashara na kazi za mikono (UTICA), shirikisho la watetezi wa haki za binadamu Tunisia (LTDH) na chama cha wanasheria Tunisia.

Mashirika hayo manne yalikuwa miongoni mwa mashirika na watu 273 walioteuliwa kuwania tuzo hiyo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Papa francis ni miongoni mwa watu mashuhuri waliopigiwa upatu kushinda.

''Mashirika haya yanashirikisha sekta tofauti za maadili katika mashirika ya kijamii Tunisia. Maisha ya ajira, maslahi, sheria na haki za kibinaadamu," amesema mwenyekiti wa kamati hiyo ya Nobel Kaci Kullmann Five.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maandamano ya Tunisia

Ni kutokana na hilo ndiposa wanne hawa walichukua majukumu yao kama wapatanishi ili kusukuma gurudumu la demokrasia na maendeleo nchini Tunisia kwa ari na maadili ya hali ya juu.

Kundi hilo lilitoa njia mbadala ya kuendeleza siasa kwa njia ya amani wakati ambapo taifa hilo lilikuwa limekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hatua yao ilitoa fursa katika kuiwezesha Tunisia, katika kipindi cha miaka michache, kuanzisha serikali ya kikatiba inayowapatia raia wake haki zao za kibinadamu bila kufuata jinsia, siasa ama hata dini.

Amesema kuwa kamati hiyo ya Nobel ina matumaini kwamba tuzo hiyo itachangia katika kulinda demokrasia nchini Tunisia bali na kutoa msukumo kwa wale ambao wanataka kuimarisha amani na demokrasia Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na dunia nzima kwa jumla.

Ushindi wa mashirika hayo ulipokelewa kwa shangwe na raia na viongozi nchini Tunisia.