Mshindi wa tuzo kuu ya Nobel kutangazwa

Papa Francis Haki miliki ya picha EPA
Image caption Papa Francis alichangia sana kurejeshwa kwa uhusiano kati ya Cuba na Marekani

Papa Francis na Angela Merkel ni miongoni mwa watu wanaopigiwa upatu kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel ambayo mshindi wake atatangazwa leo asubuhi nchini Norway.

Uwezekano wa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis kushinda umeimarishwa na juhudi zake za kupinga silaha za nyuklia na mchango wake katika kupatanisha Marekani na Cuba, kwa mujibu wa kituo cha habari cha serikali cha NRK nchini Norway.

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel, anapigiwa upatu kutokana na msimamo wake kuhusu mzozo wa wahamiaji wanaoingia Ulaya.

Lakini huwa vigumu sana kutabiri uamuzi wa kamati inayoamua mshinsi.

Wengine wanaowania tuzo hiyo ni:

  • Mussie Zerai, kasisi kutoka Eritrea aliyanzisha shirika linaloshughulikia wakimbizi
  • Denis Mukwege, daktari wa masuala ya uzazi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye ametibu maelfu ya watu waliobakwa na magenge
  • Clive Stafford-Smith, mtetezi mkongwe wa haki za kibinadamu ambaye pia ni wakili.

Miongoni mwa watu wengine mashuhuri waliopendekezwa kupigania tuzo hiyo ya £700,000 ($1.1m; €950,000) ni:

  • Edward Snowden, mfanyakazi wa zamani wa NSA aliyefichua kuhusu mipango ya udukuzi ya Marekani.
  • John Kerry na Javad Zarif, mawaziri wa mashauri ya kigeni waliofanikisha mkataba wa kihistoria kuhusu silaha za nyuklia.
  • Shirika la madaktari wasio na mipaka Medecins Sans Frontieres, kwa juhudi zake kukabiliana na mkurupuko wa Ebola Afrika Magharibi.

Watu 273 na mashirika wamependekezwa kuwania tuzo hiyo na washindi wa zamani, viongozi wa kisiasa na watu wengine mashuhuri.

Tuzo ya mwaka jana ilishindwa na mwanaharakati wa kutetea elimu Pakistan Malala Yousafzai, na mtetezi wa haki za watoto India Kailash Satyarth.

Wengine waliowahi kushinda tuzo ya Amani ya Nobel ni rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela, Rais wa Marekani Barack Obama, the Dalai Lama na kiongozi wa upinzani wa Burma Aung San Suu Kyi.

Mwaka 2012 tuzo hiyo ilikabidhiwa Muungano wa Ulaya kutambua juhudi zake katika kuendeleza Amani na maridhiano, demokrasa na haki za kibinadamu Ulaya.