Uchaguzi Guinea ni leo

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Vyama vya upinzani vilikuwa vimetoa wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi huo

Wananchi wa Guinea wanapiga kura leo kumchagua rais wao.

Kuna wagombea 7, wanaoshindana na Rais Alpha Conde, ambaye anataraji kushinda muhula wa pili.

Kampeni zilikuwa na mapambano baina ya upinzani na wafuasi wa serikali, ambapo watu kadha waliuwawa.

Guinea ndio mwanzo imeibuka kutoka janga la Ebola, ambayo iliuwa watu zaidi ya elfu-mbili; na ili kuzuwia ugonjwa huo kutapakaa, wapigaji kura wameombwa waoshe mikono kwenye maji yenye chlorine, kabla ya kupiga kura.

Awali Kiongozi wa chama cha upinzani huko Guinea, Cellou Diallo, aliwahimiza wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kupiga kura leo baada ya mahakama ya katiba nchini humo kukataa pendekezo la kuahirisha uchaguzi huo.

Image caption Uchaguzi unafanyika leo.

Vyama vya upinzani vilikuwa vimetoa wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi huo kutokana na matatizo ya kimsingi kama vile kutokamilika kwa sajili ya wapiga kura .

Upinzani ulitaka uahirishwe ilikutoa nafasi kwa tume huru ya uchaguzi kusafisha sajili hiyo kwa kuhakikisha wale walioko na kadi ya kupiga kura pekee ndio wanaosalia humo.

Aidha walitaka idadi ya wapiga kura waliojiandikisha iwekwe wazi baada ya kufuta wale walioaga dunia na wale waliojiandikisha mara zaidi ya moja.

Hapo jana muungano wawaniaji 7 wa kiti cha urais walitoa tamko la kutotambua matokeo ya uchaguzi wakidai kuwa tume huru ya uchaguzi nchini humo ilikuwa na nia ya kumsaidia rais aliyeko madarakani kusalia humo.

Viongozi hao walidai kuwa CENI (Independent National Electoral Commission) ilikuwa imepanga vituo vya kupigia kura zaidi ya kilomita tano hadi 40 katika maeneo yenye wafwasi wa upinzani huku maeneo yanayodhaniwa kuwa yanamuunga mkono rais Conde yakiwa na vituo karibu zaidi na makaazi ya watu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Hapo jana muungano wawaniaji 7 wa kiti cha urais walitoa tamko la kutotambua matokeo ya uchaguzi wakidai kuwa tume huru ya uchaguzi nchini humo ilikuwa na nia ya kumsaidia rais aliyeko madarakani

Hadi sasa CENI imeshindwa kutoa majina ya watoto ambao inadaiwa walipewa kadi za kupigia kura kinyume cha sheria.

Watu watatu washafariki katika makabiliano baina ya wafuasi wa rais aliyeko madarakani Alpha Conde na wanaharakati wa upinzani.

Kuchaguliwa kwa rais Alpha Conde miaka 5 iliyopita kuliendeleza urudishwaji wa utawala kutoka mfumo wa kijeshi na kuleta mfumo wa kiraia.