Zimbwabwe: Palmer hatashtakiwa

Image caption Daktari Palmer anaelezwa kuwa alikuwa na vibali halali vya uwindaji

Daktari wa meno ambaye alisababisha hali ya taharuki baada ya kumuua Simba mmoja mashuhuri nchini Zimbabwe hatashtakiwa kwa kuwa alikuwa na kibali cha kuwinda.

Walter Palmer alikubali kumuua Simba aitwaye Cecil lakini alikana kutekeleza shughuli za uwindaji kinyume cha sheria.

Waziri wa Mazingira wa Zimbabwe Oppah Muchinguri alisema Palmer hawezi kushtakiwa kwa kuwa alikuwa na vibali vyote.

Pia Bibi Muchinguri amesema Zimbabwe itatathimini upya namna inavyotoa leseni za uwindaji.

Awali Waziri huyo alitaka Palmer afunguliwe mashtaka, hata hivyo ilibainika kuwa hakuna sheria iliyovujwa alipomuua Simba.

Wakati huohuo kesi ya mwongozaji wa Palmer wakati wa uwindaji Theo Bronkhurst inatarajiwa kuendelea siku ya Alhamisi.

Bronkhurst amekana mashtaka kuwa alishindwa kuzuia uwindaji haramu.

Palmer akiongea kwa mara ya kwanza kuhusu tukio la mwezi uliopita ameliambia shirika la AP na Gazeti la Minneapolis Star kuwa angemfahamu Mnyama huyo kuwa muhimu kwa Zimbabwe , asingemuua.

Palmer amekuwa akizongwa sana kutokana na tukio hilo na kusema kuwa binti yake na mkewe pia wamekuwa wakitishiwa katika mitandao ya kijamii.

Palmer anaelezwa kulipa kiasi cha Dola 50,000 ili kuwinda simba katika hifadhi kubwa ya Zimbabwe