Wakazi wampiga na kumuua meya Guatemala

Guatemala
Image caption Huwa nadra sana kwa kiongozi aliyechaguliwa kushambuliwa

Wakazi katika mji mmoja nchini Guatemala wamemshambulia na kumuua meya wakimtuhumu kwa kuagiza kushambuliwa kwa mpinzani wake.

Meya Basilio Juracan alifariki baada ya kupigwa na kuchomwa na raia hao mjini Concepcion, mkoa wa Solola, mnamo Jumapili.

Wakazi wanaamini alihusika katika shambulio la awali ambapo wanawake wawili waliuawa na wengine watano kujeruhiwa.

Guatemala ni moja ya mataifa hatari zaidi Amerika Kusini na visa vya uhalifu wa kutumia silaha huwa vingi sana.

Hata hivyo, kuuawa kwa kiongozi aliyechaguliwa na wananchi si jambo la kawaida.

Mwezi uliopita, Bw Juracan alimshinda Lorenzo Sequec kwenye uchaguzi wa meya wa mji wa Concepcion, kilomita 100 magharibi mwa mji mkuu wa Guatemala City,

Baada ya kushindwa, Bw Sequec alimtuhumu Bw Juracan kwa usimamizi mbaya na akaitisha uchunguzi kuhusu matumizi ya fedha za mji huo.

Jumatatu asubuhi, Bw Sequec na jamaa zake walikuwa wakisafiri gari lao lilipofungiwa na gari jingine. Watu wasiojulikana walifyatulia risasi gari lake na binti yake wa miaka 17 na mpya wake waliuawa. Bw Sequec alijeruhiwa.

Baada ya habari za kisa hicho kuenea, kundi la wakazi wenye hasira lilimsaka Bw Juracan likidai alihusika katika shambulio hilo.

Baada ya kuteketeza nyumba kadha za jamaa za Bw Juracan, walimpata meya huyo nyumbani kwake.

Walimtoa nje, wakampiga na kumchoma.