Kiongozi wa waasi atishia kufufua vita Sudan Kusini

Sudan Kusini
Image caption Kiongozi wa Sudan Kusini Salva Kiir alitia saini mkataba wa amani Agosti 26

Kiongozi mmoja wa waasi nchini Sudan Kusini ametishia kuanza tena mapigano, licha ya mkataba wa amani uliotiwa saini wiki sita zilizopita.

Jenerali Johnson Oloni amesema Serikali imekuwa ikihujumu mkataba wa amani kwa kushambulia raia na kubadilisha mipaka ya majimbo ya nchi hiyo.

Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni kuachwa bila makao kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivoanza 2013.

Sudan Kusini ilijipatia uhuru wake kutoka Sudan miaka mine iliyopita.

Jenerali Oloni ameambia BBC kuwa huenda mkataba wa Amani usifaulu.

Alisema amekasirisshwa sana na anachodai ni wanajeshi wa serikali kukalia maeneo ambayo ni ya watu wa kabila lake.

Alisema pia amekasirishwa na mpango uliotangazwa mapema mwezi huu na Rais Salva Kiir, wa kuongeza idadi ya majimbo nchini humo hadi 28.

Jenerali Oloni amesema huo ni mpango wazi wa kudhibiti zaidi mamlaka, mwandishi wa BBC Tim Franks anaripoti.

Kiongozi huyo wa waasi amesema unyakuzi wa ardhi ndio uliofanya watu wa kabila lake kuanza mapigano miaka ya nyuma na wako tayari kupigana tena.

Mapigano yalichipuka Sudan Kusini Desemba 2013 baada ya Bw Kir kumtuhumu Riek Machar, aliyekuwa makamu wake, kwa kuandaa jaribio la mapinduzi ya serikali.

Bw Machar alikanusha madai hayo, lakini aliunda kundi la wapiganaji ambao walipigana na wanajeshi wa serikali hadi kutiwa saini kwa mkataba wa amani mwezi Agosti.