Chuo kikuu chafungwa baada ya mwanafunzi kufariki Kenya

Maseno
Image caption Chuo kikuu cha Maseno kimekumbwa na misukosuko siku za hivi karibuni

Chuo kikuu kimoja nchini Kenya kimefungwa baada ya mwanafunzi kufariki wakati wa makabiliano kati ya wanafunzi na polisi Jumatatu usiku.

Kaimu Naibu Chansela wa chuo kikuu hicho cha Maseno, magharibi mwa Kenya ameagiza chuo hicho kifungwe mara moja.

Bi Catherine Muhoma amesema uamuzi wa kufunga chuo kikuu hicho umechukuliwa baada ya kubainika hali chuoni haingeweza kudhibitiwa tena.

“Kufuatia matukio yaliyojiri usiku ambayo yalipelekea kufariki dunia kwa mwanafunzi mmoja na makabiliano kati ya wanafunzi na polisi leo asubuhi, hali imekuwa tete na hatari kwa masomo,” alisema kupitia taarifa.

“Baraza la seneti la chuo hiki limeamua chuo kifungwe mara moja. Wanafunzi wanafaa kuondoka chuoni katika muda wa dakika 30”.

Ghasia zilianza baada ya polisi kudaiwa kufyatulia risasi gari lililokuwa likitumiwa na wanafunzi kupigia debe mmoja wa wagombea katika kampeni za uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi chuoni, kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya.

Mwanafunzi mmoja alifariki akipelekwa hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga mjini Kisumu. Wanafunzi sita walijeruhiwa na kupelekwa hospitali zilizoko karibu na chuo kikuu hicho.

Mapema leo, wanafunzi walifunga barabara ya Kisumu-Busia na kulemaza uchukuzi.

Mmoja wa wanafunzi chuoni humo aliyezungumza na BBC alisema wengi wa wanafunzi wameondoka chuoni baada ya agizo la kufungwa kwake kutolewa.

Wengi hata hivyo walitatizika kusafiri nyumbani.

"Kwetu ni mbali na sikuwa nimejiandaa kusafiri. Kwa sasa nimo kwa rafiki yangu,” Bi Macharia, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne, ameambia BBC.

Wiki iliyopita, moto ambao chanzo chake hakijabainika uliteketeza sehemu ya afisi za utawala katika chuo kikuu hicho.

Uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi katika chuo kikuu hicho ulipangiwa kufanyika Oktoba 16.