Aliyegoma kula ahofiwa afya yake Angola

Image caption Mwanamuziki Luaty Beirao amekuwa akikosoa Serikali ya Angola

Afya ya mwanamuziki maarufu wa miondoko ya kufokafoka nchini Angola na mwanaharakati Luaty Beirao,ambaye alikuwa kwenye mgomo wa kutokula kwa siku 23 imekuwa mbaya.Mke wake ameeleza.

Beirao alikamatwa na Watu wengine 14 mwezi Juni wakishutumiwa kupanga mipango ya kumuondoa Rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu Eduardo dos Santos.

''nina wasiwasi kuhusu afya yake na kitakachomkuta hapo baadae'' mke wa mwanamuziki huyo, Monica Almeida aliiambia BBC.

Takriban watu 20 walikamatwa siku ya jumatatu mjini Luanda walipokuwa wakidai wanaharakati hao waachiwe huru.

Polisi walizingira kundi lao walipokusanyika katika kanisa wakiwa wamebeba mishumaa.Walishinikiza kuachwa huru kwa watu hao ambao wamekuwa wakishikiliwa kwa miezi mitatu sasa bila kufunguliwa mashtaka, ambapo ni kinyume cha Sheria nchini humo.

Mwanamuziki huyu amekuwa akiikosoa Serikali akitoa wito kutaka mgawanyo wa haki wa utajiri wa mafuta nchini humo.