Mkuu wa polisi Uganda akemewa

Image caption Afisa mkuu wa polisi Kale Kayihura

Raia wa Uganda wameingia mtandaoni wanatumia kitambulishi mada cha #SomeonetellKayihura kulalamikia kisa ambapo polisi wanadaiwa kumvua nguo mwanamke mmoja mwanachama wa chama cha upinzani cha FDC.

Kulingana na mwandishi wa BBC nchini Uganda Siraj Kalyango, mwanamke huyo alikuwa miongoni mwa wafuasi wa mgombea wa upinzani Kizza Besigye ambao walikuwa wakielekea katika mkutano wa kisiasa.

Inadaiwa kuwa maafisa wa polisi waliwasimamisha wakiwaambia mkutano huo haukuwa halalai na walipokataa wakaamua kuwakamata kwa nguvu.

Ni wakati huo ambapo mwanamke huyo aliyekuwa miongoni mwa wafuasi hao alitakiwa ajisalimishe lakini naye alipokataa maafisa wa polisi walijaribu kumbeba kwa nguvu na hapo akaishia kuvuliwa nguo.

Hata hivyo walifanikiwa kumtia ndani ya gari ya polisi akiwa nusu uchi.

Baada ya picha za kisa hicho kusambazwa katika mitandao ya kijamii, baadhi ya wanaharakati wa kijamii wakiwemo wananchi wamejitokeza na kulaani kitendo hicho.

Wanaharakati hao wanataka polisi waliomdhalilisha mwanamke huyo kuchukuliwa hatua kali.