Marekani yatuma wanajeshi Cameroon

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Vikosi vya Cameroon vimekuwa vikipambana na Boko Haram

Rais wa Marekani, Barack Obama ametangaza kuwa vikosi vya marekani vyenye silaha vimepelekwa Cameroon kusaidia mapambano dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram.

Kikosi cha wanajeshi 300, kitafanya operesheni za upelelezi, kijasusi na operesheni za kipelelezi katika ukanda mzima.

Cameroon na Chad zimekuwa zikilengwa na wanamgambo hao kutoka kaskazini mwa Nigeria.

Obama amesema vikosi hivyo vitaendelea kubaki Cameroon mpaka watakapokuwa hawahitajiki tena.

Marekani imetambua ongezeko la tishio ambalo washirika wake na nchi ambazo Marekani ina maslahi zinakabiliwa nalo kutoka kwa Boko haram pamoja na kuwa majeshi ya Cameroon, Chad,Niger na Nigeria yamekuwa yakifanya operesheni ya pamoja dhidi ya wanamgambo hao.

Mwaka jana ndege za upelelezi za Marekani na Wanajeshi waliingia kaskazini mashariki mwa Nigeria baada ya kutekwa nyara kwa zaidi ya wanafunzi wa kike 200 ambao bado hawajapatikana.