Somalia na Sudan Kusini zachapwa 4-0

Kombe la Dunia Haki miliki ya picha EPA
Image caption Ilikuwa mara ya kwanza kwa Sudan Kusini kushiriki mechi za kufuzu Kombe la Dunia

Timu za taifa za Somalia na Sudan Kusini zilicharazwa 4-0 kwenye mechi za marudiano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia zilizochezwa Jumanne.

Matokeo hayo yalifikisha kikomo ndoto za mataifa hayo za kufuzu kwa fainali hizo zitakazochezewa nchini Urusi 2018.

Niger walipata ushindi rahisi wa 4-0 dhidi ya Somalia na kufanikisha ushindi wa jumla wa 6-0.

Mahamane Cisse na Moussa Maazou anayechezea soka ya kulipwa Uchina walifunga mabao mawili kila mmoja. Niger watakutana na Cameroon raundi ya pili ya kufuzu.

Mauritania pia walipata ushindi wa 4-0 mjini Nouackchott Jumanne na kufuta ndoto ya Sudan Kusini ya kusonga, matokeo ya jumla yakiwa 5-1 kufuatia sare mechi ya kwanza.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Sudan Kusini jushiriki kampeni ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Mabao ya Mauritania yalifungwa na Moulaye Khalil, Boubacar Bagili, Moussa Samba Moussa na Ismail Diakite.

Sudan Kusini walicheza dakika 11 za mwisho wakiwa na wachezaji 10 baada ya Aluck Akeuch Deng kulishwa kadi nyekundu.

Mauritania watakutana na Tunisia raundi inayofuata.

Botswana nao walisonga kwa ushindi wa jumla wa 5-1 dhidi ya Eritrea, baada ya ushindi wa 2-1 mjini Francistown, na sasa wanajiandaa kukutana na Mali.

Burundi pia walisonga baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Seychelles mjini Bujumbura, uliowapa ushindi wa jumla wa 3-0.

Fiston Abdul Razak alifunga mabao yote mawili na sasa Burundi watakutana na DR Congo raundi inayofuata.

Kwingineko, Namibia walitoka nyuma na kucharaza Gambia 2-1 na kupiga hatua kwa ushindi wa jumla wa 3-2.

Madagascar walitoka sare 2-2 na Jamhuri ya Afrika ya Kati na wakasonga kwa ushindi wa jumla wa 5-2.

Kenya na Tanzania tayari zimefuzu kwa raundi hiyo, Taifa Stars wakipangiwa kukutana na Algeria nao Harambee Stars wakipewa Cape Verde.