Ukawa na CCM hawajathibitisha mdahalo wa urais

Image caption Mgombea wa urais wa chama cha Ukawa Edward Lowasa

Ikiwa bado takribani wiki moja kufanyika kwa mdahalo wa wagombea Uraisi nchini Tanzania,Chama tawala cha CCM na chama kikuu cha upinzani Chadema hawajathibitisha kama wagombea wao watashiriki katika mdahalo huo.

Wakizungumzia maandalizi ya mdahalo huo wakurugenzi wa mashirika yanayoandaa mdahalo huo kutoka shirika la Tanzania Media Fund(TMF),Tanzania Women’s Association (Tamwa) na Twaweza wamesema kuwa hadi sasa ni vyama vitatu tu ambavyo vimethibitisha wagombea wake kushiriki.

Wamevitaja vyama hivyo vitatu kuwa ni Alliance for Demokratic Changa (ADC),ACT Wazalendo na Chama Ukombozi wa Umm (Chaumma).

Image caption Mgombea wa urais wa chama cha CCM Dkt John Pombe Magufuli

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la TWAWEZA Aidan Eyakuze amesema kuwa mialiko ilipelekwa kwa wagombea wote Tanzania bara na visiwani.

Bw.Eyakuze amesema kuwa hii fursa ya pekee kwa vyama vyote kushiriki katika tukio hili ambalo analiita kuwa ni la kihistoria katika mdahalo ambao wanaweza kuutumia kuelezea sera za serikali zao mbali na kile watakachowatendea wananchi iwapo watawapa ridhaa ya kutawala Tanzania baada ya tarehe 25 Oktoba.

Hata hivyo mkurugenzi huyo wa TWAWEZA amewataka wananchi kuwasilisha maswali yao dhidi ya wagombea wao wa

urais ambayo yanatakiwa kutumwa na kuwafikia ifikapo siku ya ijumaa Octoba 15.2015.

Image caption Wagombea wengine wamethibitisha kushiriki mdahalo huo wa kipekee

Maswali hayo kwa mjibu wa mmoja wa waandaji hao wa mdahalo huo amesema kuwa yanaweza kutumwa kwa njia mitandao ya kijamii ama anuani yao ya ya barua pepe.

Mkurugenzi wa shirika la TMF Ernest Sungura yeye amesema kuwa walilazimika kuanzisha mdahalo huo baada ya kufuatilia na kusikia ahadi za wagombea na vipaumbele vyao.

Katika uchaguzi huu Lowassa anachuana vikali na Dkt Magufuli miongoni mwa wagombea wengine Janken Kasambala wa NRA, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Fahy Dmovutwa wa UPDP, Maximillian Lymo wa TLP, Lutasola Yemba wa ADC na Hashim Rungwe wa chama cha Chaumma.