Je,utakubali mshahara wako kukatwa na kupewa mzazi wako?

Image caption Sera ya heshima kwa wazazi Uchina

Sera isio ya kawaida na ambayo imeanzishwa na kampuni moja nchini Uchina kwa wafanyikazi kutoa kiwango kidogo cha mishahara yao kwa wazazi wao imezua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii.

Gazeti la kila siku la Guangzou limeripoti kwamba kampuni hiyo ya ususi ambayo jina lake limebanwa inataka kuonyesha maadili mema miongoni mwa wafanyikazi wake.

Heshima kwa wazazi ni miongoni mwa maadili muhimu katika jamii ya Uchina pamoja na utamaduni wake.

Lakini habari hiyo iliochapishwa na vyombo vya habari ,imezua mjadala wa iwapo kampuni hiyo imevuka mpaka.

Wazazi wengi wa Uchina wanataraji kupokea kiwango kidogo cha mshahara wa watoto wao wakati wanapoanza kulipwa.

Mwaka 2013,Uchina ilipitisha sheria inayolenga kushinikiza heshima kwa wazazi ikiwaagiza wale wanaoishi mbali na wazazi wao kuwatembelea kila mara.

Kampuni hiyo inaondoa asilimia 10 ya mshahara wa wafanyikazi ambao hawajaingia katika ndoa na asilimia tano kwa wale walioko katika ndoa kila mwezi na kuzituma moja kwa moja kwa wazazi wao.

Lakini pia huwafidia wafanyikazi,yuan 100 kwa wale walioanza kazi na Yuan 300 kwa wale waliofanya kazi kwa miaka mitatu ama hata zaidi.

Kampuni hiyo pia huwafanyia mafunzo ya kila mara wafanyikazi ambapo hufunzwa miongoni mwa maswala mengine kuhusu heshima kwa wazazi wao.