Mbunge afariki katika ajali ya ndege Tanzania

Deo Filikunjombe Haki miliki ya picha Parliament of Tanzania
Image caption Filikunjombe alikuwa safarini kutoka Dar es Salaam hadi Ludewa

Mbunge wa eneo la Ludewa aliyekuwa anamaliza muda wake, amefariki kwenye ajali ya ndege iliyotokea Alhamisi.

Bw Deo Filikunjombe alikuwa safarini kutoka jiji la Dar es Salaam kuelekea jimbo lake la Ludewa ajali ilipotokea.

Alikuwa miongoni mwa abiria wanne kwenye ndege hiyo.

Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda (Mb) anasikitika kutangaza kifo cha Mbunge anayemaliza muda wake (Jimbo la Ludewa) Mhe. Deo Filikunjombe, kilichotokea jana kwa ajali ya Ndege (Helicopter).

“Ajali hiyo ... ilitokea jana jioni tarehe 15 Oktoba, 2015 wakati Helicopter waliyokuwa wakisafiria kutokea Jijini Dar es Salaam kuelekea Jimboni kwake Ludewa kuanguka katika Hifadhi ya Selous Maeneo ya Msolwa Mkoani Morogoro,” unasema ujumbe uliowekwa kwenye tovuti ya bunge la nchi hiyo kutangaza kifo chake.

Bw Filikunjombe alizaliwa mwaka 1972 na alichaguliwa mbunge wa eneo la Ludewa lililoko mkoani Njombe mwaka 2010.

Mbunge huyo alikuwa anatetea kiti hicho uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.

Yeye ndiye mbunge wa pili aliyekuwa akiwania katika uchaguzi ujao kufariki baada ya Abdallah Kigoda wa eneo bunge la Handeni Mjini, Tanga kufariki Oktoba 12 akitibiwa nchini India.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi tayari imetangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa ubunge katika eneo la Handeni. Uchaguzi wa udiwani na urais hata hivyo utaendelea.