Wanawake maskini huvuta sigara zaidi wakiwa wajawazito

sigara Haki miliki ya picha IAN HOOTONSCIENCE PHOTO LIBRARY
Image caption Uvutaji wa sigara hudhuru mtoto aliye tumboni mwa mama

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha tofauti kubwa katika idadi ya wanawake wanaovuta sigara wakiwa na mimba nchini Uingereza, maeneo maskini yakiwa na idadi ya juu.

Takwimu hizo zinaonyesha 20.2% ya wajawazito eneo la Blackpool huvuta sigara katika kipindi cha ujauzito wao ikilinganishwa na 2.1 eneo la matajiri la Westminister.

Kila mwaka zaidi ya mimba 70,000 huathiriwa na uvutaji wa sigara.

Kwa jumla kiwango cha kadiri cha uvutaji sigara kimepungua chini ya asilimia 11 nchini Uingereza lakini ripoti ya shirika la Smoking in Pregnancy Challenge inapendekeza viwango hizo chini ya asilimia sita ifikapo 2020.

Profesa Russel Viner wa chuo cha udaktari cha watoto kiitwacho Royal Colledge Child Health amesema viwango vya uvutaji sigara miongoni mwa wanawake wachanga wenye mimba imo juu zaidi.

"Wana uwezekano mara sita zaidi wa kuvuta sigara wakiwa waja wazito wakilinganishwa na wanawake waliopitisha umri wa miaka 35.”

"Pia tunajua kuna tofauti kubwa ya kikanda na viwango vya juu zaidi vimo katika jamii fukara. Tunafaa kuchukulia suala hili kwa uzito."

Daktari wa uzazi wa chuo cha Royal College of Obstetricians David Richmond amesema ni muhimu sana kwa wanawake wajawazito kuacha kuvuta sigara wanaposhika mimba.

”Hili husaidia kuboresha afya ya mtoto, kukua kwa mtoto huyo na pia kupunguza matatizo ya ujauzito yanayoweza kuepukika," amesema.