Msomali aliyetaka kutoa mimba Australia akanusha kubadili nia

Nauru Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jumatatu, wanaopinga mpango wa kuzuilia wakimbizi Nauru waliandamana kuitaka Australia ifunge kituo hicho

Mwanamke Msomali aliyekuwa amepelekwa Australia akatoe mimba amekanusha madai kwamba alibadili nia yake baada ya kufika huko.

Mwanamke huyo anadai alishika mimba baada ya kubakwa akiwa katika kisiwa cha Nauru ambacho hutumiwa kuzuilia wakimbizi kabla yao kuruhusiwa kuingia Australia.

Alikuwa amepelekwa nchini Australia kutolewa mimba hiyo lakini alirejeshwa ghafla Nauru bila kumuona daktari.

Huwa ni haramu kuavya mimba katika kisiwa cha Nauru.

Mwanamke huyo anatafuta hifadhi nchini Australia.

Waziri wa Uhamiaji wa Australia Peter Dutton amekanusha madai ya mwanamke huyo.

Waziri huyo awali alikuwa amedai mwanamke huyo alibadili nia yake na kuamua kutotoa mimba hiyo baada ya kuwasili Australia.

Serikali ya Australia huwa na sheria kali za kuzuia wakimbizi kuingia.