Kimbunga chawahangaisha maelfu ya Wafilipino

Image caption Maelfu ya watu wahangaika na kimbunga Ufilipino

Waokoaji nchini Ufilipino wanatatizika kuwaokoa maelfu ya watu wanaokisiwa kuwa wamehamishwa makwao na mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini humo kufuatia kimbunga cha Koppu kilichoikumba tangu hapo jana.

Kimbunga hicho kinachosonga kwa kasi ya chini mno kimesababisha mvua kubwa mno.

Inaripotiwa kuwa maji yamefikia kimo cha mita nne katika sehemu zingine huku kiwango cha mvua kikiendelea kuongezeka.

Maafisa wanasema kwamba watu kadhaa wamekwama juu ya paa za nyumba zao, wakisubiri kuokolewa.

Magari ya kijeshi hayawezi kufikia maeneo hayo, huku kukiwa na upungufu mkubwa wa maboti ya ukoaji.

Haki miliki ya picha video
Image caption Magari ya kijeshi hayawezi kufikia maeneo hayo, huku kukiwa na upungufu mkubwa wa maboti ya ukoaji.

Maelfu ya watu tayari wamekimbia makwao na kuelekea kwenye maeneo yaliyoinuka na salama .

hadi kufikia sasa watu 9 wanasemekana kufariki na wengine kadhaa hawajulikani waliko.

Kimbunga hicho kiitwacho Koppu kimepungua kidogo, lakini kinatabiriwa kuwa kitaendelea kwa siku mbili zijazo.

Mkurugenzi wa shirika la msalaba mwekundu nchini Ufilipino bwana Richard Gordon amesema kuwa tayari wameshatuma maboti ya uokozi ilikuwanusuru wale waliokwama.

Taharuki kubwa imeshuhudiwa kaskazini mwa nchi hiyo, mahala ambapo kimbunga kikali kinapiga kisiwa kikuu cha Luzon, kikiandamana na mvua kubwa.