Muungano wa upinzani wasitisha kampeni TZ

Image caption Marehemu Emmanuel Makaidi

Muungano wa vyama vya upinzani nchini Tanzania UKAWA umeamua kusitisha shughuli zake zote za kampeni kwa muda ili kushiriki maziko ya mwenyekiti mwenza wa Umoja huo Dr Emmanuel Makaidi ambaye alifariki wiki iliyopita katika Hospitali ya Nyagao Mkoani Lindi Kusini mwa Tanzania kutokana na shinikizo la damu.

Umoja huo ambao kwa sasa unawakilishwa na Edward Lowassa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Tanzania, umesema kuwa marehemu ni mtu ambaye ameshiriki katika siasa za upinzani kwa muda mrefu ambapo alisimamia misimamo yake bila kuogopa jambo lolote hivyo ataendelea kukumbukwa kama mmoja wa wapenda mapadiliko nchini humo.

Maziko ya Dr Makaidi yanafanyika leo jijini Dar es Salaam katika makaburi ya Sinza baada ya mwili wake kuagwa katika viwanja vya lililokuwa Bunge la Zamani, Karimjee Hall.

Makaidi alizaliwa Aprili 10, 1941 huko wilayani Masasi mkoani Mtwara. Alianza elimu katika Shule ya Msingi Namalenga wilayani Masasi kati ya mwaka 1948 – 1952, mwaka 1953 – 1954 Middle school ya Luatala,Masasi. Mwaka 1953 hadi 1956 alijiunga na Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph na kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne.

Image caption Kiongozi wa UKAWA akihutubia umati wa watu katika kampeni za uchaguzi wa urais nchini Tanzania

Kutokana na ufaulu wake wa juu kwa msaada wa kanisa alijiunga na shule ya Sekondari ya Luhule, nchini Uganda kati ya mwaka 1957 – 1958 ambako alisoma darasa la 13 na 14.

Baadaye alijiunga na chuo Kikuu cha Witwatersrand Afrika ya Kusini na kuhitimu shahada ya uendeshaji na usimamizi kati ya mwaka 1958 – 1960 kisha akaelekea Marekani ambako aliendelea kusoma mpaka shahada ya uzamivu yaani PhD katika sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha Howard.

Alipata nafasi nyingine ya kusomea stashahada ya kuchakata taarifa za Kielektoniki katika Chuo Kikuu cha Trinity, Ireland na kukamilisha masomo yake 1977 kabla ya kurudi Tanzania kulitumikia taifa na baadaye kuingia katika Siasa.

Tanzania inategemea kufanya uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani Jumapili ya tarehe 25 mwezi huu.