Upinzani washinda uchaguzi Canada

Justin Trudeau Haki miliki ya picha AFP
Image caption Trudeau ni mwanawe aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo marehemu Pierre Trudeau

Chama cha upinzani nchini Canada cha Liberal kimeshinda uchaguzi mkuu na kufikisha kikomo uongozi wa karibu mwongo mmoja wa chama cha Conservative.

Chama hicho kinachoegemea siasa za mrengo wa kati, chini ya uongozi wa Justin Trudeau, kilianza kampeni kikishikilia nafasi ya tatu kwa mujibu wa kura za maoni lakini sasa kimeongoza kwa kura.

Bw Trudeau, 43, ambaye ni mwana wa aliyekuwa waziri mkuu Pierre Trudeau, amesema raia wa Canada walipigia kura mabadiliko halisi.

Waziri Mkuu Stephen Harper wa chama cha Conservative amekubali kushindwa na kusema atang’atuka.

Kampeni za uchaguzi mwaka huu zilikuwa ndefu zaidi na wengi walidhani kungekuwa na ushindani mkubwa.

Lakini baada ya vituo vya kura kufungwa, Bw Harper alisema alikuwa tayari amempongeza Trudeau, akisema chama cha Conservative kinakubali matokeo "bila kusita”.

Akihutubia wafuasi wa chama hicho wenye furaha baada ya ushindi, Bw Trudeau alisema Canada ilituma ujumbe wazi kwamba ni wakati wa mabadiliko.

"Tuliushinda woga kwa matumaini, tulishinda ukosefu wa Imani kwa bidii. Muhimu zaidi tulishinda wazo kwamba raia wa Canada wanafaa kuridhika na machache waliyo nayo,” alisema.

Ni wachache sana waliotarajia chama cha Liberal kushinda kwa viti vingi. Lakini matokeo ya awali yanaonyesha watapata viti 184 vya ubunge, ikilinganishwa na viti 36 pekee walivyoshinda mwaka 2011.

Haki miliki ya picha
Image caption Chama cha LIberal kimeahidi kutekeleza mabadiliko halisi

Chama hicho ndicho cha kwanza Canada kutoka nambari tatu na kushinda uchaguzi.

Chama cha mrengo wa kushoto cha New Democratic Party (NDP) kinatarajiwa kushinda viti 44, chini ya nusu ya viti kilivyokuwa navyo bunge linaloondoka.

"Nilimpongeza Bw Trudeau kwa mafanikio haya makubwa," amesema kiongozi wa NDP Tom Mulcair.