Machafuko zaidi yaripotiwa Congo Brazzaville

Haki miliki ya picha Voice of Congo
Image caption Upinzani waitisha maandamano zaidi Congo

Polisi nchini Congo Brazzaville wamefyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji walioitikia mwito wa upinzani wa kuendelea na siku ya pili ya maandamano ya kupinga nia ya rais aliyeko madarakani Denis Sassou Nguesso kuwania muhula wake wa tatu.

Waandamanaji wameweka vizuizi barabarani huku wakipigana na maafisa wa usalama.

Maeneo ya Kusini mwa jiji hilo la Brazzaville ndio lililoathirika zaidi na makabiliano hayo baina ya waandamanaji na polisi.

Makabiliano zaidi yameripotiwa katika mji mkuu wa kibiashara wa Pointe Noire.

Raia wanaoandamana wanaitikia mwito wa kiongozi wa upinzani Pascal Tsaty Mabiala aliyewataka wajitokeze kwa wingi kupinga mipango hiyo ya kubadilisha katiba ilikumruhusu rais Sassou Nguesso kuwania muhula wa tatu.

Haki miliki ya picha
Image caption Kiongozi wa upinzani Pascal Tsaty Mabiala aliyewataka wajitokeze kwa wingi kupinga mipango hiyo ya kubadilisha katiba

Tsaty Mabiala wa chama cha kidemokrasia cha PanAfrican Union for Social Democracy amesema kuwa nia yake ni kusimamisha kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika siku ya jumapili.

Tsaty Mabiala amewataka wafuasi wake wajitokeze kwa wingi mabarabarani.

Kwa siku ya pili mfululizo, mtandao wa simu na huduma za intaneti zimekatwa.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa watu wanne waliuawa baada ya polisi kuingilia kati ili kuvunja maandamano hayo ya jana.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sassou Nguesso ambaye anaumri wa miaka 72 ameiongoza taifa hilo kwa zaidi ya miaka 32 katika awamu mbili.

Mwandishi aliyeko huko amesemakuwa mji huo umezingirwa na maafisa wa usalama.

Hakuna magari mabarabarani wala shughuli za kibiashara za kiraia zimesimamishwa.

Sassou Nguesso ambaye anaumri wa miaka 72 ameiongoza taifa hilo kwa zaidi ya miaka 32 katika awamu mbili.

Katiba ya nchi hiyo inapendekeza mtu atakayewania urais wa taifa hilo asiwe na umri unaozidi miaka 70.

Vilevile rais hastahili kusalia madarakani kwa zaidi ya mihula miwili.